BEKI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Abdallah Kheri maarufu kama Sebo, ameondoka nchini leo Jumapili tayari kuelekea jijini Cape Town, Afrika Kusini kwa matibabu ya goti.

Kheri ambaye ni mmoja wa wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, alipata majeraha hayo, alipokuwa akicheza mechi ya utangulizi ya timu ya vijana ‘Azam U-20’ ili kujiweka fiti baada ya kutoka kuugua malaria, ambapo alichana mtulinga wa pembeni (anterior ligament) kufuatia kutua vibaya chini wakati akiokoa mpira wa juu.

Mratibu wa timu hiyo, Phillip Alando, ameweka wazi kuwa kabla ya kufanya uamuzi wa kumpeleka huku, Sebo alifanyiwa kipimo cha M.R.I kwenye Hospitali ya Hightech na kugundulika kuwa ana tatizo kwenye goti lake la mguu wa kulia.

“Kwa hiyo uongozi uliona ni busara apelekwe Afrika Kusini (Vincent Palloti Hospital) na amesafiri leo asubuhi na daktari wetu Dr. Mwankemwa (Mwanandi) wameenda Cape Town wataenda kumfanyia vipimo kule na baada ya vipimo watatoa ripoti, nini kitafanyika kama kutahitajika matibabu zaidi wataeleza.

“Lakini ripoti kamili ya nini kimetokea au ameumia kwa kiwango gani ama atakuwa nje kwa muda gani ni mpaka tutakapopata majibu kutoka Afrika Kusini,” alisema.