BAADA ya kucheza mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) nyumbani, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa ugenini kuvaana na KMC kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kesho Jumatatu saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye mwenendo mzuri kabisa kikiwa hakijapoteza mchezo wowote katika mechi 15 za ligi ilizocheza hadi sasa ikiwa na pointi 39 kileleni baada ya ushindi wa mechi 12 na sare tatu.

Wababe hao kutoka Chamazi kwenye viunga vya Azam Complex, wametoka kushinda mechi tisa mfululizo za ligi, ambapo katika mchezo wa mwisho imeichapa Mbao mabao 4-0, mabao yakifungwa na Joseph Mahundi aliyetupia mawili, mengine yakifungwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Nahodha, Agrey Moris.

KMC ambayo inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 17, imetoka kupata sare ya ugenini ilipocheza na Mwadui (1-1), mchezo uliopigwa Uwanja wa Mwadui Complex, mkoani Shinyanga.

Wachezaji wa Azam FC wanaotarajia kukosekana kwenye mchezo huo ni beki Abdallah Kheri, ambaye ni majeruhi, wengine ni wagonjwa wa muda mrefu Nahodha Msaidizi, Frank Domayo ‘Chumvi’, Daniel Amoah, Joseph Kimwaga, Paul Peter, ambao wanaendelea vema na programu za mwisho za kurejea uwanjani.

Beki wa kushoto Bruce Kangwa, aliyekusanya kadi tatu za njano naye atakosa mchezo huo akitumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja baada ya kukusanya idadi hiyo ya kadi, ambapo nafasi yake inatarajia kuzibwa na Hassan Mwasapili, aliyesajiliwa msimu huu akitokea Mbeya City.

Mshambuliaji mpya wa Azam FC, Obrey Chirwa, aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo ataendelea kukosekana akisubiria usajili wake kuthibitishwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hii ikiwa ni kwa wachezaji wote waliosajiliwa katika  dirisha dogo la usajili linaloendelea hadi Desemba 15 mwaka huu.

Wakati zikiwa hazina historia ya kukutana kwenye mechi za ligi, hii itakuwa ni mara ya pili timu hizo kukutana kwenye mechi za mashindano rasmi, mara ya mwisho zilikutana msimu uliopita kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Azam FC kuibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 3-1.

Mabao ya Azam FC yalifungwa na Domayo, mshambuliaji Mbaraka Yusuph, aliyeenda kwa mkopo wa miezi sita Namungo FC ya mkoani Lindi na Yahya Zayd, aliyepigilia msumari wa mwisho na kuhitimisha ushindi huo mnono huku lile la KMC likifungwa na Mohamed Hassan kwa kichwa.