IKICHEZA soka la hali ya juu, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeichapa Mbao mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Azam FC ambayo imeshinda mechi ya tisa mfululizo ya ligi, imepanda hadi kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi 39 ikiizidi pointi moja Yanga ikiyoshuka hadi nafasi ya pili lakini ikiwa na mchezo mmoja mkononi.

Mchezo huo ulianza kwa kasi timu zote zikishambuliana kwa zamu, lakini kila upande ulionekana kumdhibiti mwenzake.

Alikuwa ni nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, aliyeanza kuwainua mashabiki wa timu hiyo dakika ya 39 kwa mpira wa adhabu ya moja kwa moja na kuiandikia bao la kwanza, adhabu hiyo ilitokana na mshambuliaji Donald Ngoma, kuangushwa nje ya eneo la hatari.

Hilo ni bao la pili la Moris kwa njia ya adhabu ndogo, lingine likiwa ni lile alilofunga dhidi ya Simba, wakati Azam FC ikishinda mabao 2-1 na kutwaa taji la Kombe la Kagame Julai mwaka huu.

Mabingwa hao waliokuwa vema kwenye  mchezo huo, walijipatia mabao matatu kipindi cha pili baada ya kuizidi Mbao kwa kiasi kikubwa huku ikipeleka mashambulizi makali ya kasi.

Dakika ya 54, winga Joseph Mahundi, aliyekuwa kwenye kiwango bora aliiandikia Azam FC bao la pili akimalizia krosi safi iliyopigwa na beki Nickolas Wadada.

Mahundi tena alirejea kambani dakika nne baadaye kwa bao safi akimalizia pasi safi ya Ngoma, likiwa ni bao lake la nne msimu huu, kabla kupika bao la mwisho la Azam FC likiwa ni la nne kwenye mchezo huo likifungwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Sure Boy ambaye yupo kwenye ubora wake hivi sasa, alionekana kuwa nyota wa mchezo baada ya kushika eneo la katikati la uwanja akishirikiana na wachezaji wenzake jambo ambalo liliwapa wakati mgumu Mbao muda wote na kujikuta ikipokea kichapa hicho.

Huo ni mchezo wa 15 kwa Azam FC msimu huu, ikiwa imeshinda mechi 12, ikipata sare tatu na huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote ikiwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne tu.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuendelea na mazoezi keshokutwa Jumapili jioni tayari kuanza maandalizi ya kuikabili KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Jumatatu ijayo saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Idd Kipagwile dk 79, Salum Abubakar, Donald Ngoma, Tafadzwa Kutinyu/Salmin Hoza dk 79, Enock Atta/Yahya Zayd dk 67