KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa vitani kuvaana na Mbao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaokaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Ijumaa saa 1.00 usiku.

Azam FC ambayo tayari imerejea mazoezini kujiandaa na mtanange huo wa kiporo, itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa Stand United mabao 3-1 katika mchezo uliopita huku Mbao ikitoka kutoka suluhu ilipochuana na Ndanda ugenini mkoani Mtwara.

Mabao ya Azam FC katika mchezo huo yaliwekwa kimiani na mshambuliaji Yahya Zayd, aliyetupia mawili na kutoa pasi ya bao lililofungwa na Enock Atta, wote wawili wakiwa kwenye kiwango kizuri kwenye mchezo huo.

Ushindi wowote dhidi ya Mbao, utaifanya Azam FC iliyo nafasi ya pili hivi sasa kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi kwani itafikisha pointi 39 na itawazidi Yanga pointi moja, ambayo kwa sasa inakamata usukani wa ligi kwa pointi zake 38.

Mbao yenyewe ipo nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi ikijikusanyia pointi 20 baada ya kushinda mechi tano, sare tano na kupoteza mechi nne ikiwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 11.

Mshambuliaji Donald Ngoma, aliyemaliza adhabu yake ya kadi nyekundu, aliyoipata wakati Azam FC ikiichapa Kagera Sugar bao 1-0, huku akiwa ni mfungaji wa bao hilo pekee la timu hiyo, atakuwa akirejea kwenye mchezo huo kuimarisha safu ya ushambuliaji.

Aidha mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Obrey Chirwa, ambaye Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) imetua mwanzoni mwa wiki hii, hataweza kuwepo kwenye mchezo huo akisubiria kutoka kwa kibali chake cha kufanya kazi nchini na usajili wake kuthibitishwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, ameshaweka wazi kuwa anachoangalia hivi sasa ni kuhakikisha kikosi chake kinapata matokeo katika mechi zote wanzoshuka dimbani ili kuendelea kupigania ubingwa wa ligi hiyo.

Rekodi zao (H2H)

Kihistoria tokea Mbao ipande daraja mwaka juzi, timu hizo zimekutana mara nne kwenye mechi za ligi, Azam FC imeshinda mara mbili zote ikiwa Uwanja wa Azam Complex, ikatoka sare mara moja na kupoteza moja.

Mchezo wa mwisho zilipokutana Azam Complex, Azam FC ilishinda mabao 2-1, mabao ya Azam FC yakiwekwa kimiani na Idd Kipagwile, aliyefunga kwa kichwa ukiwa ni mpira wake wa kwanza tokea aingie jingine likifungwa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Bernard Arthur.