KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amekiri kuwa mabadiliko aliyofanya kipindi cha pili yalibadilisha mchezo na kuifanya timu yake kuichapa Stand United mabao 3-1.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) ulifanyika Uwanja wa Azam Complex jana Jumanne usiku, ambapo Azam FC ilitoka nyuma na kupata ushindi huo mnono kwa mabao yaliyofungwa na Yahya Zayd, aliyetupia mawili na Enock Atta akitupia jingine, yote yakifungwa ndani ya dakika 25 za mwisho.

Wawili hao waliofunga mabao hayo waliingia mwanzoni mwa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Danny Lyanga na Ramadhan Singano ‘Messi’, ambao walianza dakika 45 za kipindi cha kwanza.

“Nafikiri mabadiliko mawili tuliyofanya kipindi cha pili yalileta kasi zaidi katika mchezo, upambanaji zaidi, tulipotea hasa kipindi cha kwanza mara nyingi katika umiliki wa mpira, si rahisi kucheza dhidi ya timu ambayo hucheza na wachezaji wengi nyuma ya mpira,” alisema Pluijm wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz

Alisema unapocheza na timu inayocheza nyuma zaidi ya mpira unatakiwa kucheza kwa kasi katika kusambaza mipira huku akidai kuwa mbali na hayo yote walistahili kushinda mchezo huo baada ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.

“Kwa upande mwingine unapaswa kucheza kwa kasi katika usambazaji wa mipira, mbele harakati zilikuwa si nzuri, kwa sababu ukiwa winga unapocheza dhidi ya timu za aina hiyo, unapaswa kufungua kwa haraka sana na kutokea hapo unaanza kufanya harakati kwa kuwalazimisha kwenda pembeni ya uwanja.

“Lakini baada ya yote, nafikiri tumestahili kushinda kwa vile tulitengeneza nafasi kadhaa kwenye kipindi cha kwanza na pia nafasi kadhaa baada ya kufunga mabao 3-1, lakini tunapaswa kufanyia kazi hilo,” alisema.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kuendeleza moto wake kwenye mechi za ligi hiyo, hadi sasa ikiwa haijapoteza mchezo wowote ikicheza 14, ikivuna ushindi mara 11 na kupata sare tatu ikiwa imruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi hicho cha Azam FC kitaendelea kufanya mazoezi leo Jumatano jioni kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Mbao, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex keshokutwa Ijumaa saa 1.00 usiku.