USAJILI wa mshambuliaji mpya wa Azam FC, Obrey Chirwa, umekamilika asilimia 100 baada ya Chama cha Soka nchini Misri (EFA) kuiachia Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa kuituma kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

EFA imeachia ITC yake baada ya Nogoom FC kuithibitishia kuwa wameachana na mchezaji huyo na yupo huru kujiunga na timu yoyote, ambapo wiki chache zilizopita Azam FC ilimaliza taratibu za kumuhamisha kwa kuingia naye mkataba wa mwaka mmoja.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Nurdin Amin ‘Popat’, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa tayari kibali hicho kimeshatumwa TFF na sasa wanachosubiri ni kukamilika kwa vibali vyake vya kufanya kazi nchini pamoja na leseni itakayomwezesha kucheza soka nchini.

“Tunamshukuru Mungu leo jioni (jana) TFF imetupa taarifa ya kupokea ITC ya Chirwa kutoka Misri alipokuwa akicheza awali, hataweza kuiwahi mechi ya leo kutokana na kutokuwa na leseni ya kucheza ligi na kibali chake cha kufanya kazi kutokamilika, tunatarajia atacheza mechi ijayo ya Ijumaa dhidi ya Mbao,” alisema.