KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetumia vema dakika 25 za mwisho ikitoka nyuma na kuichapa Stand United mabao 3-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 36 ikiwa na nafasi ya pili baada ya kushinda mechi 11 na sare tatu, ikizidiwa pointi mbili na vinara Yanga waliokuwa nazo 38.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa, timu zote zikionyeshana ushindani mkubwa na haikushangaza dakika 45 za kwanza kumalizika kwa timu zote kuwa nguvu sawa, pande zote zikipoteza nafasi za kufunga mabao.

Stand United ilitangulia kupata bao la uongozi dakika ya 52 kupitia kwa Hafidh Musa, bao ambalo liliongeza kasi ya mashambulizi kwa Azam FC.

Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, ya kuwaingiza kipindi cha pili mshambuliaji Yahya Zayd na winga Enock Atta, yalizaa matunda baada ya wachezaji hao kuhusika kwenye mabao yote matatu ndani ya dakika 25 za mwisho za kipindi cha pili yaliyopindua uongozi wa Stand.

Dakika ya 65, Atta aliisawazishia Azam FC kwa bao safi la kichwa akimalizia krosi iliyopigwa na Zayd, na hilo linakuwa bao lake la kwanza msimu huu.

Alikuwa ni Atta tena aliyehusika kwa bao pili la Azam FC baada ya kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mwamuzi, Huseein Athuman, kutoka Katavi kuamuru upigwe mkwaju wa penalti uliofungwa vema na Zayd dakika ya 71.

Zayd aliihakikishia ushindi Azam FC kwa kuifungia bao la tatu dakika ya 85 akitumia vema pasi ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, likiwa ni bao lake la tano msimu huu.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuendelea na mazoezi kesho Jumatano kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Mbao utakaofanyika Ijumaa hii saa 1.00 usiku.

Kikosi Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Salmin Hoza dk 90, Salum Abubakar, Danny Lyanga/Zayd dk 46, Tafadzwa Kutinyu, Ramadhan Singano/Atta dk 46