KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa nyumbani Azam Complex kesho Jumanne kuikabili Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) unaotarajia kuanza saa 1.00 usiku.

Azam FC iliyokuwa kwenye maandalizi kabambe kujiandaa na mchezo huo muhimu kabisa wa ligi, itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi saba mfululizo za ligi ikiwa nafasi ya pili kwa pointi zake 33 nyuma ya Yanga iliyokileleni kwa pointi 35.

Mabingwa hao wa CECAFA Kagame Cup mara mbili mfululizo, kwenye mchezo uliopita wametoka kuichapa Ruvu Shooting mabao 2-1, mabao ya Azam FC wakiwekwa kimiani na winga Ramadhan Singano ‘Messi’ na kiungo mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu.

Ubora mwingine wa Azam FC ni kuwa timu pekee iliyoruhusu mabao machache kwenye ligi hiyo hadi sasa nyavu zake zikitikiswa mara tatu huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote kama vinara Yanga.

Kwa asilimia 90, Azam FC imeshamaliza maandalizi ya mchezo huo na sasa inasubiri kumaliza mazoezi ya mwisho leo Jumatatu jioni, ambapo wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri kabisa kwa ajili ya kusaka pointi nyingine tatu nyumbani.

Winga Enock Atta, aliyekuwa akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata wakati Azam FC ikikabiliana na JKT Ruvu, naye anatarajia kukiimarisha zaidi kikosi hicho akirejea baada ya kumaliza adhabu hiyo.

Aidha mshambuliaji Donald Ngoma, ataendelea kukosekana baada ya kulimwa kadi nyekundu wakati Azam FC ikiichapa Kagera Sugar bao 1-0 wiki chache zilizopita, huku akiwa ni mfungaji wa bao hilo pekee la matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex.

Kikosini wachezaji majeruhi wanaendelea kujiweka sawa kabla ya kurejea dimbani ni beki Daniel Amoah, Nahodha Msaidizi Frank Domayo ‘Chumvi’, winga Joseph Kimwaga na mshambuliaji Paul Peter.

Rekodi zilipokutana

Timu hizo kihistoria zimekutana mara sita kwenye mechi za ligi tokea Stand United ipande daraja mwaka 2015, Azam FC imeshinda mara nne na kupoteza mara mbili huku kukiwa hamna sare yoyote iliyowahi kupatikana.

Azam FC haijawahi kupoteza mchezo wowote dhidi ya Stand United, kila zinapocheza kwenye Uwanja wa Azam Complex, mara mbili ilizopoteza ilikuwa katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Stand United inakutana na Azam FC ikiwa na rekodi mbaya kila ikigusa ndani ya Uwanja wa Azam Complex, kutokana na takwimu kuonyesha kwenye mechi tatu ilizotua ndani ya dimba hili haijawahi kufunga bao lolote.

Jumla ya mabao 12 yamefungwa baina ya timu hizo zilipokutana mara zote hizo, Azam FC ikifunga asilimia 97 ya mabao hayo yote, ikitupia nyavuni mara tisa huku Stand United ikiziona nyavu za matajiri hao mara tatu tu zote ikiwa ni mkoani Shinyanga.

Mara ya mwisho zilipokutana ndani ya Azam Complex msimu uliopita, Azam FC ilishinda mabao 3-0 yaliyowekwa kimiani na kiungo Salmin Hoza, beki wa kushoto, Bruce Kangwa na aliyekuwa mshmbuliaji wa timu hiyo, Bernard Arthur.