KATIKA uboreshaji wa shughuli za kila siku za timu, uongozi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, umefanya mabadiliko kidogo kwenye timu hiyo.

Mabadiliko hayo yaliyofanyika hivi karibuni, lengo kuu ni kuongeza ufanisi kwenye uongozi wa timu hiyo ambapo hivi sasa kimeongezwa cheo kipya cha Mratibu wa timu (Team Coordinator), ambaye atahusika kuratibu shuguli mbalimbali za timu za kila siku.

Aliyekuwa Meneja wa timu hiyo, Phillip Alando, amepandishwa cheo na sasa ndiye atakuwa Mratibu wa timu huyo, huku nafasi yake ikizibwa na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Luckson Kakolaki, aliyeshika wadhifa huo kipindi cha Kocha wa zamani wa timu hiyo, Stewart Hall, miaka miwili iliyopita.

Kakolaki atakayekuwa na majukumu ya moja kwa moja ya timu kubwa, nafasi yake ya Meneja wa timu ndogo (Azam Academy) itazibwa na Rashid Said Zubery, aliyewahi kuwa mchezaji wa kikosi hicho (Azam U-20) kabla ya kupata majeraha yaliyomuweka nje ya dimba kwa muda mrefu hadi sasa.

Baada ya mabadiliko hayo, hivi sasa muundo wa uongozi wa timu hiyo ambayo hivi sasa ni Kampuni (Azam FC Limited), unaundwa na Bodi ya Wakurugenzi ambayo ipo chini ya wamiliki wa timu hiyo familia ya mmoja wa Wafanyabiashara maarufu Afrika, Said Salim Bakhresa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo akiwa ni Nassor Idrissa ‘Father’, safu ya uongozi wa timu ippo chini ya Mwenyekiti Shani Christoms, Makamu Mwenyekiti, Omary Kuwe, Ofisa Mtendaji wa timu, Abdulkarim Nurdin Amini ‘Popat’, na Mratibu wa timu, Phillip Alando.

Katika hatua nyingine, winga wa timu hiyo, Joseph Mahundi, amesaini mkataba mpya wa miaka miwili utakaomfanya kuendelea kusalia kwenye viunga vya timu hiyo hadi mwaka 2020.

Mahundi ambaye ni mchezaji wa muda mrefu wa Azam FC akianzia timu za vijana na baadaye kwenda kuzitumikia timu mbalimbali kabla ya kurejea Azam FC miaka miwili iliyopita, amekuwa kwenye kiwango bora kabisa hadi sasa msimu huu akifunga mabao mawili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).