BENCHI la ufundi la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, linafanyia kazi kasoro ndogo ndogo kwenye safu ya ushambuliaji ili kuiwezesha kufunga mabao mengi zaidi katika mechi mbalimbali wanazocheza.

Azam FC imekuwa ambayo mpaka sasa imefanya vema kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu huu ikiwa kileleni kwa pointi 33, ambapo safu yake ya ushambuliaji imeonekana kukosa nafasi kadhaa za kufunga mabao kwenye asilimia kubwa ya mechi walizocheza hadi sasa.

Ili kuondokana na tatizo hilo kwenye mechi zijazo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa wanaendelea kuwapa mazoezi maalumu washambuliaji wao kwenye programu zao za sasa ili kuwawezesha kufunga mabao.

“Tunataka tupambane kwa sababu tunajua tuna presha kubwa sana ya kuhakikisha bado tunazidi kukaa juu katika msimamo wa ligi. Tunapambana kabisa kuhakikisha tunapopata mechi tunatengeneza nafasi nyingi lakini ufungaji bado haujaturidhisha sisi walimu tunataka kuhakikisha kama magoli yanasaidia.

“Kwa sababu katika vita ya kupambana kama watu mnakuja kulingana pointi basi magoli yanaweza kukusaidia kwa hiyo tupo kwenye nafasi hiyo na tunashughulika sana kama leo (jana) unaona mazoezi ya leo tulikuwa tukijitahidi sana katika nafasi ya ushambuliaji kuhakikisha umaliziaji unafanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Akizungumzia siri ya mafanikio ya Azam FC hadi sasa msimu huu Mwambusi aliongeza kuwa; “Kikubwa tunasema kuwa ni mazoezi na mafunzo ambayo wachezaji wanajitahidi kuyashi. Kikubwa ni ushirikiano na umoja vilevile tunawashukuru viongozi na mashabiki kwa kuwa pamoja na timu.

“Na kuhakikisha tunapata mahitaji ambayo tunayahitaji kwa wakati muafaka ili kuweza kuhakikisha mapambano yetu yasiweze kuwa na kikwazo hapo njiani, kikubwa tunawaomba wazidi kutuombea dua na tushikamane kwa sababu ligi bado ndefu, ni ngumu na mpambano bado unaendelea lakini tutahakikisha tunapambana hadi dakika ya mwisho.”

Kikosi hicho kwa sasa kimeshaanza mazoezi tokea Jumatatu iliyopita, kikijiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Stand United utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumanne ijayo saa 1.00 usiku.

Azam FC imevuna pointi 33 baada ya ushindi wa mechi 10 na sare tatu ikiwa haijapoteza mchezo wowote, katika takwimu za wafungaji bora hadi sasa, kiungo wake mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu ndio kinara wa mabao ndani ya timu hiyo akiwa amefunga manne.

Wachezaji wanaomfuatia ni washambuliaji Yahya Zayd na Donald Ngoma, waliofunga matatu kila mmoja huku Joseph Mahundi na Danny Lyanga, nao kila mmoja akitupia nyavuni mara mbili.