KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimeshaanza rasmi mazoezi leo tayari kuanza safari ya kuzisaka pointi kuelekea mchezo ujao dhidi ya Stand United.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utafanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex Desemba 4 mwaka huu, ambapo Azam FC iko kwenye mwenendo mzuri baada ya kushinda mechi saba mfululizo za ligi hiyo.

Wachezaji wote wa Azam FC wameripoti mazoezini wakiwa na hali nzuri kabisa isipokuwa kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye ni mgonjwa.

Beki wa kulia Nickolas Wadada, aliyekuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa ya Uganda, naye amesharejea kundini akiwa ni miongoni mwa wachezaji walioripoti kwenye mazoezi hayo.

Kikosi cha Azam FC kinatarajia kuendelea na mazoezi kwa wiki hii yote, Jumamosi hii asubuhi kikitarajia kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya vijana ya timu hiyo (Azam U-20) kwa ajili ya kujiweka sawa.

Azam FC hadi sasa imeshacheza mechi 13 za ligi, ikiwa imesdhinda mara 10 na kutoka sare mara tatu ikijikusanyia jumla ya pointi 33 na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi.