MASHABIKI wengi wa soka wamekuwa wakiwa na maswali mengi kuhusu staili ya ushangiliaji ya winga Ramadhan Singano ‘Messi’, aliyofanya jana Alhamisi mara baada ya kufunga bao dhidi ya Ruvu Shooting.

Azam FC iliwachapa maafande hao mabao 2-1 katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), ambapo Singano maarufu kama Messi, mara baada ya kuifungia timu yake bao la kwanza alishangilia kwa kulamba kidole gumba cha mkono wake wa kushoto na kuonyesha ishara ya ‘Y’ wakati akilamba kidole hicho.

Singano akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz amesema kuwa ameshangilia bao kwa staili hiyo akimshukuru Mwenyezi Mungu baada ya kumjalia mke wake kupata mtoto wa kiume mwanzoni mwa wiki hii, akiwa ni mtoto wake wa kwanza kwenye maisha yake.

“Staili yangu ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia mke wangu kunipa mtoto wa kiume, shangilia ile ilikuwa inamaanisha herufi ya ‘Y’ jina la baba yangu Yahya na mtoto wangu nikimpa jina la Yahya Ramadhan Singano,” alisema.

Alizungumzia ushindi huo, akidai kuwa umoja na mshikamano wa Azam na mashabiki kwa ujumla ndio umewafanya kushinda mcheza huo.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 33 na kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kushinda mechi 10 na sare tatu ikwia haijapoteza mchezo hata mmoja.