BAADA ya mapumziko ya takribani wiki mbili kupisha mechi za kufuzu Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon, kikosi cha Azam FC kitashuka dimbani kuvaana na Ruvu Shooting kesho Alhamisi saa 1.00 usiku.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, unatarajia kuwa mkali na wa aina yake kutokana na ushindani wa timu zote mbili kila zinapokutana.

Kikosi cha Azam FC kina hali nzuri kabisa kuelekea mtanange huo, na itakumbukwa kuwa kinaingia kikiwa kimetoka kupata ushindi kwenye mechi sita zilizopita za ligi hiyo, tatu zikiwa za nyumbani na nyingine tatu mfululizo za ugenini.

Wachezaji wote wa Azam FC wapo kwenye hali nzuri kambini wakiendelea na maandalizi isipokuwa, ambapo jana Jumanne jumla ya wachezaji tano waliokuwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ walijiunga mazoezini na wenzao kuendelea kujiweka sawa na mchezo huo.

Nyota hao ni Nahodha Agrey Moris, Abdallah Kheri, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Yahya Zayd, ambao wameripoti wakiwa kwenye hali nzuri kabisa wakiwa na ari ya kupata matokeo mazuri katika mchezo huo.

Aidha hivi sasa wanaosubiriwa kujiunga kambini ni nyota wawili Nickolas Wadada (Uganda) na Tafadzwa Kutinyu (Zimbabwe), ambao waliokuwa kwenye timu zao za Taifa, Kutinyu akitarajiwa kujiunga leo Jumatano huku Wadada akiripoti kesho Alhamisi.

Azam FC inatarajiwa kumkosa mshambuliaji wake tegemeo, Donald Ngoma, baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Shomari Lawi, kwenye mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar, ambao walishinda ugenini kwa bao lake kipindi cha kwanza akitumia vema pasi ya Kutinyu.

Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amesema kuwa wanapaswa kufanya kila linalowezekana kupata pointi tatu kutoka na ugumu wa Ruvu Shooting.

“Nafikiri vijana wamefanya kazi vizuri sana kwa bahati mbaya sana baadhi ya wachezaji wamewasili leo (jana waliokuwa Taifa Stars) na hiyo kwao itakuwa mara ya kwanza kufanya mazoezi na timu lakini tunapaswa kujua kuwa tunatakiwa kuchukulia kwa uzito kwa sababu ninachojua kwenye historia Azam dhidi ya Ruvu.

“Ruvu ni mpinzani mgumu sana, tunatakiwa wote kujitoa, tunapaswa kufanya kila kitu kiwezekanavyo kupata pointi tatu na hilo ndilo lengo letu ikiwa tunacheza nyumbani,” alisema.

Alisema kukosekana kwa Ngoma ni nafasi na changamoto kwa mchezaji mwingine kuonyesha uwezo wake huku akidai anamkosa mchezaji ambaye amethibitisha kuwa ni hatari kwenye eneo la ushambuliaji akiwa tayari ameshafunga mabao matatu.

“Ushindani upo kwa washambuliaji wetu, hivi karibuni Chirwa (Obrey) anaweza kuwa tayari kutumika baada ya mechi kadhaa lakini jambo la muhimu tunaloliongelea hivi sasa ni mchezo wa Alhamisi ijayo (kesho) dhidi ya Ruvu na kila mmoja anapaswa kuwa sehemu ya mchezo huo,” alisema.

Wakati timu hizo zikienda kupambana, kihistoria zimekutana mara 14, ambapo Azam FC imeshinda mara nane, ikifungwa mara moja na mechi tano zilizobakia zikiisha kwa sare.

Rekodi zinaonyesha kuwa katika mechi hizo ambazo Azam FC ilishinda, ni mechi tatu tu zilizoisha kwa mabingwa hao kutoka uwanjani wakiwa wamefunga bao moja, ambapo zingine zote zilizobakia ilipata ushindi wa wastani wa kuanzia mabao mawili hadi manne.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana msimu uliopita, Azam FC ilishinda bao 1-0 nyumbani kwa bao safi la dakika za mwisho lililofungwa na mshambuliaji Yahya Zayd, huku matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex wakipoteza kwenye Uwanja wa Mabatini kwa kuchapwa mabao 2-0.

Kwenye mechezo huo wa kwanza kupoteza dhidi ya Ruvu Shooting, Azam FC ililazimika kucheza pungufu kipindi cha pili baada ya mwamuzi wa mchezo huo, Shomari Lawi, kumuonyesha kadi ya pili ya njano na nyekundu nahodha Agrey Moris.

Ikiwa imetoka kuifunga timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23 ‘Ngorongoro Heroes’ mabao 2-0 kwenye mchezo wa kirafiki, timu hiyo inayodhaminiwa vinywaji safi kutoka Bakhresa Food Products, juisi za African Fruti na maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, Azam FC itaingia uwanjani ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi zake 30.

Katika takwimu za mechi zote walizocheza, Azam FC imefanikiwa kushinda mara tisa na kupata sare tatu huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja na ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili na timu pinzani.