KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imehamishia rasmi Uwanja wa Taifa mechi zake za nyumbani itakazocheza na Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu huu.

Katika barua iliyoandikwa jana kuelekea Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) na nakala yake kutumwa kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeeleza kuwa sababu kubwa ya Azam FC kufikia uamuzi huo ni kuwapa nafasi mashabiki wengi kushuhudia mechi hizo kutokana na udogo wa Uwanja wa Azam Complex.

“Uongozi wa Azam Football Club unaomba ofisi yako tukufu kurejesha mechi zetu za Ligi Kuu za nyumbani zinazohusisha timu za Simba na Yanga zichezwe katika Uwanja wa Taifa msimu huu 2018/2019 badala ya kuchezwa Uwanja wa wetu wa Azam Complex,” ilieleza barua hiyo.

Ikieleza sababu za kufikia uamuzi huo, barua hiyo iliyoandikwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amini ‘Popat’, ilidai kuwa; “Hii ni kutokana na uwezo mdogo wa uwanja wa Azam Complex kuingiza mashabiki na watazamaji.”

Aidha barua hiyo pia ilieleza changamoto walizopata kwenye mechi za kwanza zilizofanyika msimu uliopita ndani ya uwanja huo, wakidai kuwa idadi kubwa ya mashabiki walikosa fursa ya kutazama mechi hizo mbili dhidi ya Simba na Yanga jambo ambalo si zuri kwa maendeleo ya mpira wa miguu.

Azam FC ikiutumia kwa mara ya kwanza uwanja wake kwenye mechi hizo mbili, iliweza kutoka suluhu dhidi ya Simba kabla ya kupoteza kwa mabao 2-1 walipocheza na Yanga, bao la matajiri hao likifungwa na Shaaban Idd nay ale ya Yanga yakifungwa na mshambuliaji, Obrey Chirwa, aliyehamia Azam FC wiki iliyopita na beki wa zamani wa Azam FC, Gadiel Michael.