KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imejidhatiti kufanya kweli kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Ruvu Shooting utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Novemba 22 mwaka huu saa 1.00 usiku.

Ili kujiandaa vema na mchezo huo tayari kikosi cha Azam FC kimeshaanza mazoezi tokea juzi Jumatatu na wachezaji kuingia kambini, ili kujiweka sawa na mchezo huo muhimu.

Ligi hivi sasa imesimama kwa takribani wiki mbili kupisha mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon, Tanzania ‘Taifa Stars’ ikitarajia kucheza dhidi ya Lesotho Jumapili hii.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa malengo yao ni kupambana kwenye mchezo huo na kuhakikisha wanafanya vizuri.

“Sisi kama timu lazina tujiandae na mazoezi yaendelee kama kawaida kwa sababu mapumziko ni kwamba ligi imesimama lakini sio timu kufanya mazoezi kwa hiyo tunaendelea na mazoezi yetu kama kawaida kwa ajili ya kuwajenga kiari wachezaji, kimwili na kimazoezi kuweka mwili sawasawa na kimbinu zaidi.

“Kwa sababu tunajua tuna mechi yetu ya kiporo tarehe 22 na Ruvu Shooting kwa hiyo majaliwa yetu ni kuhakikisha tunapambana katika mechi hiyo kufanya vizuri,” alisema.

Alisema licha ya hapa katikati kutokea matatizo ya kuondokewa na shabiki wao (Fetty Azam), wao kama Azam FC wamejipanga kwa umoja kuhakikisha wachezaji wa timu hiyo wanakuwa na moyo wa kuipigania timu.

“Tunaongoza msimamo wa ligi kila timu inayokuja kupambana na sisi itataka kutusimamisha au kutupunguza tusiende na kasi yetu lakini kikubwa tunajua lengo letu ni nini na tunahitaji nini,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Mbeya City na Tanzania Prisons, alisema kuwa mapumziko hayo yanawapa nafasi nzuri kama makocha kufanya marekebisho kikosini huku akidai kuwa kwa sasa wanashughulikia tatizo la kutofunga mabao mengi kwenye eneo la ushambuliaji.

“Sisi inatupa nafasi nzuri ya kuweza kurekebisha makosa ukijua tumeweza kushinda ugenini lakini tumepata magoli kiasi goli moja goli moja lakini tunashukuru kwa kupata pointi tatu kikubwa tunafanyia kazi katika eneo hilo sasa ili tunapopata timu ya kucheza nayo tuweze kufunga mabao zaidi ya moja kwa sababu mnaweza kulingana pointi lakini magoli yakazidi kwa hiyo itasaidia magoli mbele ya safari,” alisema.

Aidha katika kujiandaa vilivyo dhidi ya maafande hao, Mwambusi amedhibitisha kuwa Azam FC itacheza mchezo mmoja wa kirafiki utakaowapa mwangaza kabla ya kuvaana na Ruvu Shooting.

Azam FC imeanza mazoezi ikiwa na mshambuliaji wake mpya, Obrey Chirwa, atakayeongezwa kwenye usajili wa dirisha dogo unaofunguliwa kesho Alhamisi, akisajiliwa akitokea Nagoon FC ya Misri aliyovunja nayo makataba baada ya makubaliano ya pande zote mbili.

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex kwa sasa wapo kileleni mwa msimamo wa ligi, wakiwa na pointi 30 baada ya kushinda mechi tisa na sare tatu ikiwa haijapoteza mchezo wowote na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.