KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefikia makubaliano na kuingia mkataba wa mwaka mmoja na mshambuliaji Obrey Cholla Chirwa.

Chirwa aliyewahi kukipiga Platinums FC ya Zimbabwe na Yanga, anatua Azam kwenye usajili wa dirisha dogo unaofunguliwa Novemba 15 mwaka huu, akitokea Nagoon ya nchini Misri aliyovunja nayo mkataba baada ya timu hiyo kukiuka matakwa ya mkataba wake.

Ujio wa Chirwa atakayekuwa akivali jezi namba saba, ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm, aliyekuwa akimhitaji ili kuboresha eneo la ushambuliaji.

Mshambuliaji huyo raia wa Zambia, kwa mara ya nyingine anaungana na mshambuliaji Donald Ngoma, waliowahi kufanya kazi pamoja wakiwa Platinum na Yanga pamoja na kocha Pluijm aliyewahi kumfundisha akiwa Yanga.

Akizungumzia usajili wake mbele ya waandishi wa habari wakati akitambulishwa, Chirwa aliahidi kufunga mabao ndani ya timu hiyo huku akidai atafurahi zaidi kama timu hiyo itachukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).

“Nifuatilie nitakapoanza kucheza, mimi  nitafunga mabao 10 na hapo katika magoli 10 nitafunga hat-trick mbili au tatu nifuatilie vizuri sana,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Nashukuru Mungu viongozi wameshanipa mkataba wa mwaka mmoja pia na mashabiki wa Azam waniombee vizuri na timu ifanye vizuri ichukue ubingwa msimu huu mimi kikubwa nataka kuongea sana nakuja kupambana Azam ichukue ubingwa ndio kikubwa mimi nilichokuwa nacho.”

Naye Kocha Pluijm akizungumzia usajili wake, alisema kuwa Chirwa ni aina ya mchezaji ambaye ataongeza kitu kwenye timu hiyo pamoja na kuisaidia.

“Najua mwenendo wake, tabia yake, najua ubora wake, ni mchezaji anayeweza kuisaidia timu ni mchezaji mwenye moyo wa bidii, tokea alipoondoka Yanga nilikuwa nikiwasiliana naye…ninachojua tukiwa na Chirwa tuna uwezo mkubwa kwenye ushambuliaji.

“Ni mchezaji mzuri, ana ubora ninaotaka kuuona kwa mshambuliaji, ana spidi, anapambana, hakubali kushindwa na hiyo ndio morali tunayohitaji unapotaka kushinda kitu kwenye timu,” alisema.

Zoezi hilo la kutambulishwa Chirwa, lilihudhuriwa na viongozi wa Azam FC akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin ‘Popat’, Meneja wa timu, Phillip Alando.