KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendeleza wimbi la ushindi mara sita mfululizo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera leo saa 8.00 mchana.

Huo ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Azam FC ugenini ikitoka kuzichapa JKT Ruvu (1-0), Singida United (1-0) kabla ya leo kuinyuka Kagera Sugar na kuwa timu ya kwanza kuichapa timu hiyo nyumbani kwake msimu huu.

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, wanafanikiwa kufikisha jumla ya pointi 30 na kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kushinda mechi tisa na sare tatu ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja huku ikiwa imeruhusu mabao mawili tu ya kufungwa.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, aliwaanzisha kwa pamoja viungo washambuliaji Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Tafadzwa Kutinyu, huku akimsogeza pembeni Yahya Zayd, aliyekuwa akishambulia kutokea upande wa kushoto na mara kadhaa akibadilishana upande wa kulia na winga Joseph Mahundi.

Mchezo huo ulikuwa ni wa ushindani kwa pande zote mbili, ambapo ilibidi Azam FC isubirie hadi dakika tano za mwisho za kipindi cha kwanza kuweza kuandikisha bao hilo la ushindi lililowakikishia pointi tatu muhimu.

Dakika ya 41 Sure Boy aligongeana vema na Kutinyu, aliyempa pasi ya mwisho mshambuliaji Donald Ngoma na kuandika bao hilo kabla ya mpira kwenda mapumziko, Azam FC ikiwa kifua mbele kwa bao hilo.

Hilo ni bao la tatu kwa Ngoma kwenye ligi hiyo msimu huu, baada ya kuzitikisa pia nyavu za Coastal Union na Singida United, ambapo kwa sasa analingana mabao na wachezaji wenzake Zayd na Kutinyu.

Azam FC ilijitahidi kucheza vema kipindi cha pili na kufanikiwa kulinda ushindi huo, safu ya ulinzi chini ya nahodha Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, kipa Razak Abalora na kiungo mkabaji Mudathir Yahya, ikifanya kazi kubwa kuokoa hatari zote za Kagera Sugar.

Mabingwa hao wa Kagame Cup na Mapinduzi Cup mara mbili mfululizo, wanaodhaminiwa na vinyaji safi kutoka Bakhresa Food Products; juisi za African Fruti na maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents Tanzania Limited, walipata pigo dakika ya 90 baada ya mwamuzi Shomari Lawi, kutoa kadi nyekundu iliyoshangaza wengi kwa mshambuliaji Donald Ngoma.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho Jumatatu, tayari kuanza maandalizi ya mechi nyingine zijazo, ikianza na mechi ya kiporo dhidi ya Ruvu Shooting Novemba 22 mwaka huu, itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Idd Kipagwile dk 88, Salum Abubakar, Donald Ngoma, Tafadzwa Kutinyu, Yahya Zayd/Danny Lyanga dk 72