BENCHI la ufundi la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, limejipanga vilivyo kuwajenga wachezaji kisaikolojia na kisawasawa ili kuendelea na rekodi nzuri waliyoanza katika Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu huu.

Azam FC iliyoichapa Kagera Sugar leo bao 1-0 lililofungwa na Donald Ngoma, ipo kileleni kwa takribani wiki nne sasa ikifikisha jumla ya pointi 30 baada ya ushindi wa mechi tisa na sare tatu huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi, alisema kuwa bado hawajaridhika wao kama benchi la ufundi na wachezaji kwani malengo yao ni kufika pale walipokusudia.

“Tunashukuru mwenendo tunaoendelea kwenda nao na ushindi, ligi bado ndefu hatujaridhika bado hatujaridhika sisi kama makocha tunataka nia yetu tufike pale tulipokusudia na wachezaji vilevile hawajaridhika ina maana kila mechi inayokuja mbele yetu ni fainali tunataka pointi tatu,” alisema.

Alisema wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufakisha kupata pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar huku akiwapongeza wachezaji na viongozi kwa ushirikiano wa pamoja uliofanikisha kupatikana kwa ushindi huo.

“Licha ya mazingira magumu tuliyopangiwa kucheza saa 8, si muda mzuri kutokana na hali ya hewa iliyopo hapa (Bukoba) ni joto na wakati mwingine tulitegemea mvua lakini leo haikuwepo na kulikuwa na hali ya joto kubwa sana kiasi kwamba wachezaji ni binadamu wanakwenda sehemu vifua vinafunga.

“Tuliweza kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu sana tunasema kucheza na timu kama Kagera timu ambayo inakaa watu tisa nyuma ya mpira kila wakati ni ngumu sana kuweza kupata magoli mengi lakini niwashukuru wachezaji wameweza kupambana tumeweza kupata goli moja na kulilinda mpaka dakika za mwisho,” alisema.

Akizungumzia kadi nyekundu aliyoonyeshwa Ngoma dakika za mwishoni za mchezo huo, Mwambusi alisema wanahitaji kujiridhisha juu ya kadi hiyo kutokana na mazingira aliyotoa mwamuzi wa mchezo huo, Shomari Lawi.

“Tumeweza kumaliza mchezo salama pamoja na kupata kadi ambazo zinasikitisha hasa kadi nyekundu aliyopata Ngoma na kadi nyingine za njano ambazo kwa kweli tunawaambia wachezaji mara nyingi waweze kuwa na nidhamu ya mchezo.

“Lakini kadi nyekundu bado tunakuwa hatujui ni kwanini imetoka lakini tutafuatilia na viongozi tutawaambia wafuatilie kwa sababu mchezaji kapewa kadi nyekundu yuko ndani ya uwanja lakini hatujui kilichotokea pale ni nini amemkanyaga mchezaji wa timu ya Kagera au yametokea majibizano ya namna gani hayo tutayajua baada ya kufuatilia,” alisema.

Aidha akizungumzia walivyojipanga kuendelea na rekodi nzuri waliyokuwa nayo, Mwambusi alisema: “Kikubwa tunamuomba Mwenyezi Mungu kwa sababu huu ni mpira tunacheza na timu ambazo zimejiandaa vema kwamba sio kila siku tutakuwa katika kiwango ambacho tunacho lakini kikubwa tunataka tuwajenge wachezaji kisaikolojia wawe vizuri wawe kisawasawa kuhakikisha tunaendeleza rekodi na kucheza vema na kushinda michezo inayokuja mbele yetu.”

Mara baada ya kumaliza mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kucheza mechi nyingine ya ligi Novemba 22 mwaka huu dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Katika hatua nyingine, kwa sasa ligi hiyo itasimama kwa siku takribani 18 kupisha mechi za kufuzu Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon, ambapo Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajia kukipiga na Lesotho ugenini Novemba 18 mwaka huu.

Wachezaji wa Azam FC walioitwa kuunda kikosi cha timu hiyo ni mabeki Nahodha Agrey Moris, Abdallah Kheri, viungo Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na mshambuliaji Yahya Zayd.

Nyota wengine wa kimataifa wa Azam FC walioitwa timu za Taifa, ni beki Nickolas Wadada, aliyeitwa Uganda ‘The Cranes’ inayotarajia kucheza na Cape Verde pamoja na kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu, aliyejumuishwa katika kikosi cha Zimbabwe.