KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa na kazi nzito kesho Jumapili itakapokuwa ugenini kuvaana na Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera kuanzia saa 8.00 mchana.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa inataka kuendelea wimbi la ushindi kwa mechi ya sita mfululizo, ili kuendelea kusalia kileleni mwa ligi hiyo hadi sasa ikijikusanyia jumla ya pointi 27 kufuatia ushindi wa mechi nane na sare tatu.

Ikionyesha imedhamiria kupata ushindi katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kiliwasili mjini Bukoba tokea Jumatatu iliyopita (Oktoba 29) kikiwa kina morali kubwa ya kuzoa pointi zote tatu.

Wakati Azam FC ikipata ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo uliopita dhidi ya Singida United, wapinzani wao Kagera Sugar wametoka kupoteza pointi tatu ugenini baada ya kufungwa bao 1-0 na ndugu zao, Mtibwa Saugar.

Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, ameweka wazi kuwa wachezaji wake na morali kubwa kutokana na aina ya matokeo mazuri wanayoendelea kuyapata.

“Tuna nafasi kubwa kwa sababu tumeshinda mechi zetu mbili za mwisho za ugenini, hii ndiyo ya mwisho (Kagera Sugar) na kwa matumaini tunaweza kufanya tena kwa sababu kuna hali nzuri sana kwenye kundi, wako tayari kwa ajili ya kufanya kazi na hilo ndio jambo la muhimu.

“Pia tunajua ubora wa Kagera wanapocheza nyumbani, timu inyotumia nguvu, ina wachezaji wenye nguvu na ndio maana unatakiwa kuruhusu mpira uende na pia kumiliki mpira na wakati kuna nafasi ya kufunga unatakiwa kutumia nafasi hizo bila shaka na kufunga mabao pia kama unataka kushinda,” alisema.

Naye Nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, alisema wanajua kuwa mchezo huo utakuwa mgumu lakini wao kama wachezaji wamejipanga kupata matokeo mazuri.

“Naiheshimu Kagera Sugar siku zote wakicheza na sisi wanaonyesha upinzani ila na sisi kwa upande wetu kama Azam tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo, tulichopanga kuendeleza ni kuhakikisha kila mchezo uliopo mbele yetu tunashinda tutajua mwisho wa msimu tupo katika nafasi gani,” alisema.

Kuelekea mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaendelea kuwakosa wachezaji wake beki David Mwantika, Nahodha Msaidizi, Frank Domayo ‘Chumvi’, winga Joseph Kimwaga, washambuliaji Mbaraka Yusuph, Ditram Nchimbi na Wazir Junior, ambao ni majeruhi huku Enock Atta, akiendelea kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata dhidi ya JKT Ruvu.