WAKATI zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya kikosi cha Azam FC haikijakabiliana na wenyeji wao Kagera Sugar, Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati wameendelea na maandalizi makali kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakopigwa Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Azam FC iliyowasili mkoani humo tokea Jumatatu iliyopita usiku, imemaliza programu ya mazoezi kwa siku ya tatu ikijiandaa vilivyo na mchezo huo huku ikijipanda kuendeleza wimbi la ushindi.

Mabingwa hao hadi sasa wanashikilia usukani wa ligi wakiwa na pointi 27 baada ya ushindi wa mechi nane na sare tatu ikiwa haijapoteza hata moja, ambapo imetoka kushinda michezo mitano mfululizo ikiwemo miwili ya ugenini dhidi ya JKT Ruvu (1-0) na Singida United (1-0).

Kagera Sugar iliyopoteza mechi moja kati ya 11 ilizocheza hadi sasa, inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo ikiwa na pointi zake 16, zilizotokana na ushindi wa mechi tatu na sare saba.

Kuelekea mchezo dhidi ya Kagera Sugar, zifuatazo ni takwimu muhimu za timu hizo tokea zilipoanza kukutana kwenye ligi msimu wa 2008-2009, Azam FC ilipopanda daraja na kuanza kucheza rasmi Ligi Kuu.

Rekodi muhimu (2008-2018)

Huo utakuwa ni mchezo wa 21 kihistoria tokea zianze kukutana Ligi Kuu, katika mechi 20 zilizopita, Azam FC imeonekana kuwa na wastani mzuri ikiwa imeshinda mara 10, ikipoteza mara tano huku michezo mitano ikiisha kwa sare.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye Uwanja wa Kaitaba, mchezo uliisha kwa sare ya bao 1-1, bao la Azam FC likifungwa kwa ufundi mkubwa na winga machachari, Idd Kipagwile, aliyeuzungusha mpira pembeni kidogo ya lango na kujaa wavuni.

Katika mechi tisa zilizopita dhidi ya Kagera Sugar, Azam FC imeonekana kufanya vizuri baada ya kushinda mara saba huku Kagera Sugar ikishinda moja na kutoka sare moja, ikiwa ni rekodi nzuri kwa upande wa mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Kombe la Kagame na Kombe la Mapinduzi.

Mara ya mwisho Azam FC kupoteza mchezo kwenye Uwanja wa Kaitaba, ilikuwa ni miaka nane iliyopita (Septemba 15, 2010), Kagera Sugar ikishinda bao 1-0, tokea hapo imefanikiwa kucheza mechi sita mfululizo ndani ya uwanja huo bila kupoteza ikishinda mara tatu na sare tatu.

Mechi nyingine moja ya ugenini iliyobakia inayokamilisha mechi saba mfululizo kwa Azam FC kutopoteza ugenini dhidi ya Kagera Sugar, ilifanyika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga wakati wa ukarabati wa Uwanja wa Kaitaba, na Azam FC kushinda mabao 2-1, yaliyofungwa na Nahodha wa zamani wa timu hiyo, Himid Mao ‘Ninja’ aliyetimkia Petrojet ya Misri na Kipre Tchetche anayekipiga Terengganu ya nchini Malaysia hivi sasa.

Jumla ya mabao 51 yamefungwa kwenye mechi zote 20 walizokutana kwenye ligi, Azam FC ikifunga jumla ya mabao 31 ikiwa na wastani kufunga bao 1.6 kwenye kila mchezo, na Kagera Sugar ikitiksia nyavu za matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex mara 20.