KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Hans Van Der Pluijm, ameweka wazi kuwa kikosi chake kimestahili ushindi walioupata dhidi ya Singida United.

Kauli hiyo ya Pluijm imekuja baada ya kikosi chake kuilaza Singida United bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Namfua, mjini Singida, bao pekee la Azam FC likiwekwa kimiani na staa wa timu hiyo, Donald Ngoma.

Ushindi huo umeifanya Azam FC inayodhaminiwa na vinywaji safi kutoka Bakhresa Food Products, juisi za African Fruti na maji safi ya Uhai (Uhai Drinking Water) na Tradegents Tanzania Limited, umeifanya kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha jumla ya pointi 27, zilizotokana na ushindi wa mechi nane na sare tatu huku ikiwa haiajpoteza hata moja.

Pluijm ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo kuwa wamestahili ushindi huo hasa kutokana na wachezaji wake kujitolea kwa kupambana muda wote hadi wanafanikisha pointi tatu hizo ugenini.

“Kutoka mwanzo tulijaribu kufunga bao la mapema na pia tukafunga bao safi sana, baada ya hapo kipindi cha pili tukafanya mabadiliko kadhaa lakini sifikiri kwamba hatukupewa nafasi nyingi ikiwa tulistahili kushinda, na nafikiri tulistahili ushindi, ikiwa unashinda mechi zako hivyo unastahili kukaa kileleni,” alisema.

Akizungumzia kikosi hicho kupata ushindi wa tano mfululizo, Pluijm alisema hiyo inatokana na wachezaji kujitambua na kutolea kwenye mechi wanazocheza.

“Natoa sifa zangu zote kwa wachezaji namna wanavyofanya mazoezi, umeona hili pia jana (juzi) namna wanavyofanya kazi wako tayari kujiua wao kwa kila mmoja hili ndilo la muhimu kwenye mpira kucheza kitimu,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Singida United, Yanga, Berekum Chelsea, Ashanti Gold, hakusita kutoa shukrani zake kwa mashabiki wa timu hiyo walioweza kuwapa sapoti huku akidokeza kuwa Azam FC inastahili kupata mashabiki wengi zaidi anaowaona.

“Timu hii inastahili mashabiki zaidi ya ilionao, wanahitaji mashabiki wengi zaidi lakini niliongea kabla kuna timu mbili hapa Yanga na Simba, timu za jadi wamepata mashabiki wengi, vyombo vya habari vimekuwa vikitoa mkazo mkubwa kwao, lakini nafikiri vijana wangu (Azam FC) wanahitaji mkazo huo pia,” alisema.

Kuelekea mchezo ujao dhidi ya Kagera Sugar utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera Jumapili hii (Novemba 4), Pluijm amesema kuwa timu yake itacheza soka la kweli wanalotakiwa kuonyesha kwenye uwanja mzuri.