KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imezidi kufanya kweli kwenye mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) baada ya kuichapa Singida United bao 1-0.

Huo ni ushindi wa tano mfululizo kwa kikosi hicho, ambapo imeendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha jumla ya pointi 27 zilizotokana na ushindi wa mechi nane na sare tatu ikiwa haijapoteza hata moja.

Azam FC imepambana kweli hadi inaambulia pointi tatu hizo hasa kutokana na ushindani mkubwa waliouonesha Singida United huku hali ya Uwanja wa Namfua ukionekana kuwa mbaya na kuathiri mipango na mashambulizi ya timu zote.

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, walikitumia vema kipindi cha kwanza kwa kupata bao hilo muhimu na pekee lililofungwa na mshambuliaji Domald Ngoma, dakika ya 30 akitumia vema pasi ya juu ya mshambuliaji mwenzake, Yahya Zayd.

Hilo ni bao la pili kwa Ngoma msimu huu, la kwanza akifunga wakati Azam FC ikiilaza Coastal Union mabao 2-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex wiki chache zilizopita.

Ushindi huo unamaanisha kuwa, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amefanikiwa kuwafunga waajiri wake wa zamani aliowatumikia msimu uliopita kabla kutua kwa matajiri hao msimu huu, akiondoka na wachezaji wake watatu, kiungo Mudathir Yahya, Tafadzwa Kutinyu na mshambuliaji Danny Lyanga.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka mjini Singida kesho Jumatatu saa 12 asubuhi tayari kuanza safari ya kuelekea mkoani Kagera kukipiga na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba Novemba 4 mwaka huu saa 8.00 mchana.

Kikosi cha Azam FC leo

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Yakubu Mohammed (C), Mudathir Yahya/Salmin Hoza dk 86, Joseph Mahundi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Donald Ngoma, Yahya Zayd/Tafadzwa Kutinyu dk 65, Ramadhan Singano/Danny Lyanga dk 57