KWA mara ya pili mfululizo Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa ugenini kuvaana na Singida United kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Namfua, mkoani Singida kesho Jumapili saa 10.00 jioni.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikitoka kuichapa JKT Tanzania bao 1-0 ugenini, lililofungwa na mshambuliaji Yahya Zayd, akitumia vema pande safi la staa mwingine wa timu hiyo, Donald Ngoma.

Hadi sasa ina rekodi nzuri kabisa kwani ipo kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 24 baada ya kushinda mechi saba na sare tatu ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja na kuruhusu wavu wake kutikiswa mara mbili tu katika mechi 10 ilizocheza.

Kikosi cha Azam FC tayari kimewasili mkoani humo kikiwa na ari kubwa ya kuendeleza wimbi la ushindi kwa kuongeza pointi tatu muhimu dhidi ya Walima alizeti hao, ambapo itakuwa mara ya kwanza kwa matajiri kucheza ndani ya dimba hilo.

Msimu uliopita zilipokutana kwa mara ya kwanza baada ya Singida United kupanda daraja, mtanange baina ya timu hizo ulifanyika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, ulioisha kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, mechi iliyomtoa kinda wa Azam FC, Paul Peter, aliyeisawazishia timu yake katika mchezo wake wa kwanza.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, ameshaweka wazi kuwa licha ya ubovu wa Uwanja wa Namfua, atakipanga kikosi chake kupambana na kupata matokeo mazuri ili kuendelea kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi.

Watakaokosekana

Kuelekea mchezo huo, Azam FC inatarajia kuendelea kuwakosa wachezaji wake ambao ni wagonjwa, Nahodha Agrey Moris na Msaidizi wake, Frank Domayo, David Mwantika, washambuliaji Ditram Nchimbi, Wazir Junior, Mbaraka Yusuph na Enock Atta, atakayekuwa akitumikia adhabu yak di nyekundu aliyoipata dhidi ya JKT Tanzania.

Urejeo Namfua

Wakati Azam FC ikitumia kwa mara ya kwanza uwanja huo uliopo mjini Singida, wachezaji watatu wa Azam FC, Mudathir Yahya, Tafadzwa Kutinyu. Danny Lyanga na Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm, watacheza kwa mara ya kwanza dhidi ya timu yao ya zamani, waliyokuwa nayo msimu uliopita kabla kutua kwa matajiri hao msimu huu.

Rekodi zilipokutana

Kihistoria timu hizo zitakuwa zikikutana kwa mara ya tatu kwenye mechi ya ligi, mara mbili zilizopita Azam FC ilishinda mara moja na kutoka sare moja.

Ukiondoa sare ya bao 1-1 ugenini kwenye mchezo wa kwanza, Azam FC ilipata ushindi nyumbani Azam Complex kwa kuichapa bao 1-0 lililofungwa na winga Joseph Mahundi.

Vilevile ziliwahi kukutana kwenye nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu visiwani Zanzibar, Azam FC ikishinda bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Shaaban Idd, na kutinga fainali kabla ya kutwaa taji hilo.