KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari kipo mkoani Singida kufanya mambo makubwa kuhakikisha inaendeleza wimbi la ushindi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).

Azam FC hadi sasa ipo kwenye fomu nzuri ikiwa imecheza mechi 10 za ligi ikifanikiwa kushinda mara saba na kutoka sare tatu ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi zake 24.

Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) waliwasili salama mkoani humo usiku wa jana, wachezaji wakiwa na ari kubwa ya kufanya vema kwenye mchezo huo.

Kikosi cha Azam FC kilichowasili mkoani hapa kinaundwa na makipa Razak Abalora, Mwadini Ally, mabeki Yakubu Mohammed, Abdallah Kheri, Bruce Kangwa, Hassan Mwasapili, Nickolas Wadada, Oscar Masai, Lusajo Mwaikenda.

Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya, Salmin Hoza, mawinga ni Joseph Mahundi, Ramadhan Singano ‘Messi’, Idd Kipagwile na washambuliaji ni Tafadzwa Kutinyu, Yahya Zayd, Donald Ngoma, Danny Lyanga.

Mara baada ya Azam Fc kukabiliana na Singida United keshokutwa Jumapili, kitaondoka moja kwa moja kesho yake kuelekea mkoani Kagera kukipiga na Kagera Sugar Novemba 4 mwaka huu.