KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Hans Van Der Pluijm, ameweka wazi kuwa unapocheza ugenini cha muhimu ni kupata ushindi kuliko kuangalia namna gani ulivyocheza.

Kauli hiyo imekuja mara baada ya kuichapa JKT Tanzania bao 1-0 jana jioni ugenini lililofungwa na Yahya Zayd, kwenye mechi waliyocheza katika mazingira magumu ya uwanja pamoja na kuwa pungufu ya mchezaji mmoja kwa dakika 54 za mchezo huo.

Azam FC ilicheza pungufu baada ya winga Enock Atta, kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 36 na mwamuzi wa mchezo huo, Alex Mahagi kutoka jijini Dar es Salaam.

“Jambo la muhimu sana unapocheza mechi za ugenini kwenye viwanja kama hivi (vibovu) jambo la muhimu ni kushinda na jinsi unavyocheza sio muhimu kabisa, tulitaka kuendelea kukaa kileleni jambo muhimu tumepata pointi tatu, kwangu mimi ni muhimu sana,” alisema Pluijm wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz

Pluijm alisema anajivunia wachezaji wake kutokana na ari ya kupambana waliyoonyesha kwenye mchezo huo huku akisifia namna walivyoweza kuzuia mashambulizi yote ya JKT Tanzania.

“Najivunia wachezaji wangu kama utaona kipindi cha kwanza baada ya dakika 25 tumepata kadi nyekundu, kwa maoni yangu haikuwa kadi nyekundu lakini nataka kuangalia baadaye kwenye picha za televisheni halafu kwa namna wachezaji wetu walivyozuia nadhani sifa zote ziende kwao,” alisema.

Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Singida United, alisema wanakwenda kucheza kwenye uwanja mbaya zaidi lakini atakipanga kikosi chake kiakili kwa ajili ya kupata matokeo.

“Singida uwanja ni mbaya zaidi ya huu (Meja Gen. Isamuhyo) tunatakiwa kujiandaa kwa hilo pia, angalia kama una mtazamo sahihi na mawazo sahihi unaweza kubadilisha akili yako na ukacheza kwa namna nyingine haraka mipira mirefu, haraka kwenda mbele na pia pengine unaweza kutimiza malengo yako,” alimalizia.

Azam iliyokileleni ikiwa na pointi 24 inakabiliwa na mechi mbili nyingine za ugenini, ikitarajia kukipiga dhidi ya Singida United Jumapili hii Oktoba 28 kwenye Uwanja wa Namfua kabla ya kuelekea mjini Bukoba, Kagera kuivaa Kagera Sugar Novemba 4 mwaka huu.