LICHA ya kucheza pungufu ya mchezaji mmoja kwa dakika 54, Azam FC imeweza kunawiri baada ya kuichapa JKT Tanzania bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Meja Gen. Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.

Azam FC imecheza pungufu baada ya winga wake, Enock Atta, kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo huo Alex Mahagi kutoka Dar es Salaam.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake timu zote zikishambuliana vilivyo na kupambana kuhakikisha kila mmoja anavuna ushindi, lakini Azam FC ndio iliyoibuka mwamba ikipata bao pekee lililofungwa na mshambuliaji Yahya Zayd, dakika ya 52 akitumia vema pande safi la Donald Ngoma.

Hilo linakuwa bao la tatu kwa Zayd msimu huu, mabao yote akifunga ndani ya mechi nne zilizopita huku akiwa amechangia bao moja pia ikiwa ni rekodi nzuri kabisa.

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, wanafanikiwa kuandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kupata ushindi Ligi Kuu kwa kuwafunga wenyeji JKT Tanzania kwenye Uwanja wao huo wa Meja Gen. Isamuhyo na inakuwa timu ya kwanza kuwafunga maafande hao msimu huu.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 24 na kuzidi kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 10 za ligi ikishinda mara saba na sare tatu ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaanza safari ya kuelekea mkoani Singida kesho Alhamisi Alfajiri (Oktoba 25) tayari kukabiliana na Singida United katika mchezo ujao wa ligi utakaofanyika Uwanja wa Namfua Jumapili hii.

Kikosi cha Azam FC leo

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Yakubu Mohammed, Mudathir Yahya/Tafadzwa Kutinyu dk 85, Joseph Mahundi, Salum Abubakar, Donald Ngoma/Danny Lyanga dk 70, Yahya Zayd/Hassan Mwasapili dk 82, Enock Atta (Red Card dk 36)