KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imezidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) baada ya kuichapa African Lyon mabao 2-1 leo usiku.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 21 baada ya kucheza mechi tisa za ligi hiyo ikishinda mara sita na sare tatu huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake kutokana na upinzani wa timu hizo zinazotokea eneo moja.

Lyon ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 10 likifungwa na Hood Mayanja, aliyepiga shuti lililombabatiza (deflection) beki Abdallah Kheri na mpira kumpoteza maboya kipa Razak Abalora.

Dakika tatu baadaye Yahya Zayd, aliisawazishia Azam FC kwa bao safi akimalizia kazi nzuri ya Joseph Mahundi. Hilo linakuwa bao la pili kwa Zayd kwenye ligi msimu huu.

Azam FC iliendelea kusaka bao la ushindi, ikicheza vema na kwa uelewano mkubwa kuanzia safu ya ulinzi chini ya Nahodha Agrey Moris, safu ya kiungo iliyokuwa ikiundwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya.

Aidha safu ya ushambuliaji chini ya Donald Ngoma, Yahya Zayd, Joseph Mahundi, Enock Atta, ilionekana kufanya kazi kubwa kusukuma mashambulizi langoni mwa Lyon, ambao waliweza kuondoa hatari zote.

Baada ya kosakosa nyingi, Azam FC iliweza kujipatia bao la ushindi dakika ya 89 lilifungwa na Abdallah Kheri, kufuatia kona iliyochongwa na Yahya Zayd.

Baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho Jumamosi kabla ya kurejea mazoezini Jumapili jioni kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya JKT Tanzania utakaofanyika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Oktoba 24 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Hassan Mwasapili, Abdallah Kheri, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya/Salmin Hoza dk 84, Joseph Mahundi, Salum Abubakar, Donald Ngoma, Yahya Zayd, Enock Atta/Danny Lyanga dk 64