KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa kibaruani kupambana na African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex kesho Ijumaa saa 1.00 usiku.

Huo utakuwa ni mchezo wa mwisho kwa kikosi hicho kucheza nyumbani mwezi huu Oktoba, kwani itahamia ugenini kwa kucheza mechi nne mfululizo ikianza Na JKT Tanzania, Singida United, Kagera Sugar na Mbao.

Kikosi cha Azam FC kinaendelea na mazoezi makali, tayari kabisa kwa mtanange huo unaotarajiwa kuwa mkali kutokana na historia ya timu hizo zinazotoka eneo linalokaribiana, Azam FC ikitoka Chamazi na Lyon makazi yake yakiwa ni Mbagala.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) mara mbili mfululizo wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa kileleni katika msimamo kwa pointi zao 18 baada ya kushinda mechi tano na sare tatu huku ikiwa haijapoteza hata moja.

Wakati timu hizo zinakutana, Azam FC imetoka kushinda mabao 2-0 kwenye mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Coastal Union huku Lyon ikipoteza kwa kufungwa 2-1 walipokutana na Simba na hadi sasa ikiwa imejikusanyia pointi sita tu katika nafasi ya 18.

Wakati leo ikitarajiwa kufanya mazoezi ya mwisho leo jioni kuelekea mchezo huo, Azam FC inawatarajia mazoezini wachezaji wake saba walioko timu za Taifa, Nahodha Agrey Moris, David Mwantika, Abdallah Kheri, Mudathir Yahya, Yahya Zayd (Taifa Stars), Nickolas Wadada (Uganda) na Tafadzwa Kutinyu (Zimbabwe).

Habari nyingine njema ni jana kurejea mazoezini kwa beki wa kushoto, Bruce Kangwa, aliyekuwa kwenye maziko ya kaka yake aliyepata ajali ya kugongwa na gari nchini Afrika Kusini wiki chache zilizopita wakati Azam FC ikijiandaa na mchezo dhidi ya Biashara United.

Benchi la ufundi la Azam FC chini ya Mholanzi, Hans Van Der Pluijm, tayari limeweka mikakati kuelekea mechi hiyo, likijipanga vilivyo kuhakikisha wanaendelea na wimbi la ushindi waliokuwa nao kwenye michezo miwili iliyopita ili kuendelea kuwania taji la ligi hiyo.

Kihistoria timu hizo zimekutana mara 10 kwenye mechi za ligi, Azam FC ikiwa imeshinda mechi sita, sare tatu na kupoteza mmoja, huku jumla ya mabao 23 yakiwa yamewekwa kimiani katika michezo yote hiyo, matajiri hao wakizitungua nyavu za wapinzani wao mara 16 na Lyon ikiziona nyavu za Azam FC mara saba.

Lyon ni miongoni mwa timu nne zilizoweza kupata matokeo ya ushindi kwenye Uwanja wa Azam Complex tokea ufunguliwe mwaka 2011, ikipata ushindi huo Agosti 23 mwaka huu ikiichapa Azam FC bao 1-0 lililofungwa na Adam Kingwande, timu nyingine tatu zikiwa ni JKT Tanzania, Kagera Sugar na Yanga.

Lakini Azam FC kupoteza dhidi ya Lyon kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na kucheza pungufu kwa mchezaji mmoja muda mwingi wa mchezo huo baada ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, kuonyeshwa kadi nyakundu na mwamuzi Israel Nkongo (Dar es Salaam).

Ushindi wowote wa Azam FC kesho utaifanya kufikisha pointi 21 na kujikita zaidi kileleni, ambapo timu pekee itakayoweza kuifikia ni Yanga, ambayo ina mechi mbili mkononi huku ikiwa ina jumla ya pointi 16.