KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, asubuhi hii imewafunza soka timu yake ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Azam U-20’ baada ya kuifunga mabao 5-0 katika mchezo wa kirafiki wa mazoezi uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC ni kama imelipa kisasi kwa madogo zao kwani Jumamosi iliyopita zilicheza katika mchezo wa kwanza wa kirafiki na Azam U-20 kushinda mabao 3-2 kabla ya kurudiana leo.

Benchi la ufundi la Azam FC chini ya Mholanzi Hans Van Der Pluijm, limetumia mechi hizo mbili kama sehemu ya kukipa mazoezi kikosi chake na kuwasoma wachezaji vijana kwa ajili ya manufaa ya baadaye ya timu kubwa.

Mabao ya Azam FC yaliwekwa kimiani na beki Yakubu Mohammed na washambuliaji Donald Ngoma, Mbaraka Yusuph, Danny Lyanga na Ditram Nchimbi, aliyefunga bao la mwisho.

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye maandalizi kabambe kuelekea mechi ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya African Lyon itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex Ijumaa hii saa 1.00 usiku.

Wakati kikielekea kuhitimisha mazoezi hayo kwa siku mbili zilizobakia kabla ya mchezo huo, kikosi hicho kitarejea mazoezi kesho Jumatano jioni kikiimarishwa na nyota watano walikuwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Nahodha Agrey Moris, Abdallah Kheri, David Mwantika, Mudathir Yahya na Yahya Zayd.

Nyota wengine wawili waliokuwa timu za Taifa nje ya Tanzania, ni beki wa kulia Nickolas Wadada (Uganda), Tafadzwa Kutinyu (Zimbabwe), ambao wote saba wanakabiliwa na mechi za kufuzu Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.