WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) ikiwa imesimama, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeonekana kuwa na rekodi ya aina yake miongoni mwa timu shiriki.

Ligi hiyo imesimama kupisha mechi za kufuzu Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon, timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ikitarajia kumenyana na Cape Verde, ikicheza ugenini juzi kabla ya kurudiana nao keshokutwa Jumanne.

Azam FC imefanya mambo makubwa hadi sasa, ikiwa ipo kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 18 zilizotokana na ushindi wa mechi tano na sare tatu huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.

Mbali na rekodi hiyo, Azam FC ndio timu pekee ambayo ni ngumu kufungika hadi sasa katika mechi nane ilizocheza imeruhusu wavu wake kutikiswa mara moja tu huku ikifunga jumla ya mabao 11.

Kipa wake namba moja, Razak Abalora, amefanya kazi kubwa akiwa mwamba kwani katika mechi saba kati ya nane alizoidakia timu hiyo msimu huu amefanikiwa kuruhusu bao katika mchezo mmoja tu ukiwa ni sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Mwadui, mechi moja nyingine akidaka Mwadini Ally.

Ukiachana na ubora wa Razak, pia kuna ubora wa mabeki wanne wanaosimama mbele yake Nahodha Agrey Moris, Abdallah Kheri, Nicholas Wadada na Bruce Kangwa, mabeki wengine waliocheza nafasi ulinzi katika mechi hizi nane ni David Mwantika na Hassan Mwasapili.

Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Kagame Cup na Mapinduzi Cup, wamepania kutwaa taji la ligi msimu na hadi sasa wakionekana kufanya vema jambo ambalo linaashiria mwanga mzuri kuelekea kutimiza lengo hilo.

Mara baada ya mechi za kufuzu AFCON, Azam FC itarejea kwenye mechi za ligi kwa kucheza na African Lyon Ijumaa ijayo, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.