NYOTA wawili wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Nahodha Msaidizi Frank Domayo ‘Chumvi’ na mshambuliaji Paul Peter, wameondoka jijini Dar es Salaam leo mchana kuelekea nchini Afrika Kusini kwa matibabu.

Domayo na Peter wamepata majeraha ya goti, kiungo huyo akiumia hivi karibuni akiwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iliyokuwa ikifanya maandalizi ya kuvaana na Cape Verde huku mshambuliaji huyo naye akiumia miezi michache iliyopita akiwa na timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’.

Wawili hao wameondoka wakiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’, ambaye atashughulikia taratibu zao za kimatibabu wakati wanafanyiwa uchunguzi kwenye Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo jijini Cape Town.

Matibabu yao yanatarajia kuanza kesho Alhamisi chini ya Daktari Robert Nickolas, ambaye atarudia vipimo walivyotoka kufanyiwa jijini Dar es Salaam na kutoa muongozo wa kutibu majeraha yao.