WAKATI kikosi cha Azam FC kikirejea kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi, amesema kuwa wanategemea mambo makubwa zaidi huko mbele.

Azam FC imekaa kileleni baada ya kuichapa Coastal Union mabao 2-0 na kufikisha jumla ya pointi 18 huku ikiwa imecheza mechi nane za ligi hiyo ikishinda tano na sare tatu.

Mwambusi ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa licha ya Coastal Union kuziba njia zao lakini hawakuweza kukataa tamaa na kufanikiwa kupata mabao hayo.

“Tunamshukuru Mungu mchez ulikuwa mzuri na ulikuwa mgumu Coastal wameweza kupambana wameweza kutuzuia katika njia zetu nyingi lakini hatukuweza kukata tamaa wachezaji wameweza kuamka na tuliweza kuwakumbusha nini cha kufanya majukumu yao.

“Tukaweza kupata goli la kwanza kipindi cha kwanza na kipindi cha pili tulitengeneza nafasi nyingi tumepata goli moja kikubwa tunamshukuru Mwenyezi Mungu, tunawashukuru wachezaji kwa ukomavu wao mzuri,” alisema.

Kocha huyo alisema kwa mchezaji kama Donald Ngoma kufunga bao lake la kwanza katika mchezo huo, kutamjengea hali ya kujiamini zaidi.

Baada ya mchezo huo, ligi hiyo inatarajia kusimama kwa siku takribani 11, kupisha mechi za kufuzu Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon, ambapo Azam FC itashuka tena dimbani kupambana na African Lyon kwenye Uwanja wa Azam Complex Oktoba 19.