BAADA ya kufungua akaunti ya mabao akiwa na jezi ya Azam FC jana, mshambuliaji Donald Ngoma, amejinasibu ya kuwa kufunga ni kawaida yake.

Ngoma alifunga bao hilo dakika ya 28 na kuiongoza Azam FC kuichapa Coastal Union mabao 2-0 katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), bao jingine likiwekwa kimiani na Danny Lyanga, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mzimbabwe huyo.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Ngoma alisema kuwa anajisikia vizuri kufungua ukurasa wa mabao ndani ya timu hiyo huku akidai cha muhimu ni timu hiyo kupata ushindi.

“Kwangu kufunga ni kitu cha kawaida nimefurahi sana kwa sababu tumepata pointi tatu na ndio muhimu sana, kitu cha kwanza ukiwa straika kufunga ndio kazi yangu na nimefurahi sana kwa sababu ni timu yangu mpya na nimefurahi sana kabisa,” alisema.

Staa huyo wa zamani wa Platinum ya Zimbabwe na Yanga, alisema kuwa kitu wanachoangalia hivi sasa ni kupata ushindi kwenye mechi zijazo hadi kuchukua ubingwa wa ligi.

“Tukiendelea kucheza vizuri na kupata pointi nyingine mpaka tuchukue ubingwa ndio kitu tunachoangalia kwanza,” alimalizia mshambuliaji huyo mwneye sifa za kusumbua mabeki, upambanaji na mwenye uchu wa kufunga mabao.

Ngoma amefunga bao la kwanza akiwa na jezi ya mabingwa hao kutoka viunga vya Azam Complex, kwenye mechi yake ya tatu kucheza akitokea katika majeruhi, moja akianzia benchini na mbili mfululizo akianza kikosi cha kwanza.