USHINDI wa mabao 2-0 ilioupata Azam FC dhidi ya Coastal Union usiku huu, umeifanya kukamata usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).

Azam FC imekaa kileleni baada ya kufikisha jumla ya pointi 18, zilizotokana na ushindi wa mechi tano na sare tatu huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.

Alikuwa ni mshambuliaji Donald Ngoma, aliyeifyungulia ukurasa wa mabao Azam FC akifunga dakika ya 28 akitumia pasi safi ya kiungo Mudathir Yahya.

Bao hilo linamfanya Ngoma, kufungua akaunti ya mabao Azam FC tokea asajiliwe msimu huu ikiwa ni mechi yake ya tatu kuichezea Azam FC baada ya kutoka kwenye majeraha ya muda mrefu ya goti.

Kabla ya bao hilo, dakika ya 12 Ngoma alikaribia kuipatia bao jingine Azam FC baada ya kufanya kazi nzuri ya kuwahadaa mabeki wa Coastal na kupiga shuti lililopanguliwa wa kipa Hussein Shariff ‘Casillas’ na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Dakika ya 17 winga wa Azam FC, Enock Atta, aliyeonekana kurejea vema alifanya kazi ziada ya kuwatoka mabeki wa Coastal na kupiga shuti la chini lililogonga mwamba wa pembeni kabla ya mabeki kuondoa hatari hiyo.

Azam FC iliendelea na kasi yake ya kutaka kupata mabao zaidi, lakini safu ya ulinzi ya Coastal ilisimama vema kuondoa hatari zote na kufanya kipindi cha kwanza kuisha kwa uongozi wa bao hilo kwa mabingwa hao.

Kipindi cha pili Azam FC iliendelea na kasi yake na kutengeneza nafasi kadhaa lakini wachezaji wa Coastal Union waliendelea kulinda vema lango kwa kuondoa hatari zote.

Mabadiliko ya benchi la ufundi la Azam FC kumuingiza mshambuliaji Danny Lyanga dakika ya 65 na kutoka Ngoma, yaliongeza kasi zaidi eneo la ushambuliaji la timu hiyo.

Dakika ya 70 Lyanga aliifunga timu yake ya zamani kwa bao safi la umbali wa takribani mita 21 akitumia vema uzembe wa mebeki wa Coastal walioiokoa vibaya krosi iliyochongwa na beki David Mwantika.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kwa siku mbili kabla ya kurejea tena mazoezini Alhamisi hii kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya African Lyon utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Oktoba 19 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, David Mwantika, Hassan Mwasapili, Abdallah Kheri, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Idd Kipagwile dk 84, Salum Abubakar, Donald Ngoma/Danny Lyanga dk 65, Yahya Zayd, Enock Atta/Ramadhan Singano dk 75