KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kipo tayari kwa mapambano dhidi ya Coastal Union, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumatatu saa 1.00 usiku.

Mchezo huo ni muhimu kwa Azam FC ambayo ushindi wowote utaifanya kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha jumla ya pointi 18.

Wachezaji wote wa mabingwa hao wapo fiti kuelekea mchezo huo, unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake kutokana na Coastal Union nayo kuonekana ikiwa na matokeo mazuri hadi sasa.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, ameshaweka wazi kuwa wanataka kuendeleza ushindi tena nyumbani baada ya mchezo uliopita kuichapa Prisons bao 1-0.

“Coastal Union sio timu mbaya wamekuwa wakipata matokeo mazuri, kwangu mimi jambo la muhimu ni tunatakiwa kuendelea kuwa na malengo na kucheza mechi zote kwa kuzitilia mkazo na kwenda wote kuhakikisha tunachukua tena pointi tatu,” alisema Pluijm hivi karibuni alipozungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz

Kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na juisi safi ya African Fruti, Maji safi ya Uhai Driking Water na Tradegents Tanzania Limited, usiku huu kinatarajia kumalizia maandalizi ya mwisho na benchi la ufundi kuweka sawa mbinu zao kabla ya kuvaana na Wagosi hao wa Kaya.  

Kuelekea mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuwakosa wachezaji wake watatu wa kimataifa, kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu aliye majeruhi, beki wa kulia Nickolas Wadada, aliyeripoti kwenye timu yake ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ na Bruce Kangwa, mwenye ruhusa maalumu ya kwenda katika mazishi ya kaka yake.