ZIMEBAKIA siku mbili kabla ya kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, hakijavaana na Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).

Kuelekea mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Jumatatu ijayo saa 1.00 usiku, tunakuletea takwimu mbalimbali katika namba kuhusu mechi za timu hizo zilipokutana kwenye ligi hiyo.

Rekodi katika namba

10: Ni idadi ya mechi zote zilipokutana timu hizo kwenye mechi za ligi, mchezo wa keshokutwa ukitarajiwa kuwa wa 11.

07: Ni idadi ya ushindi iliyoupata Azam FC dhidi ya Coastal Union, ikiwa imeshinda robo tatu ya mechi hizo 10, Coastal ikishinda mmoja na mbili zikitoka sare.

22: Ni idadi ya mabao yote yaliyofungwa kwenye mechi zote zilipokwaana, asilimia kubwa ya mabao yakifungwa na matajiri hao wa viunga vya Azam Complex, ambao wameziona nyavu za Coastal mara 18 huku nayo ikiruhusu manne.

06: Ni idadi ya mabao ya mfungaji bora wa mechi baina ya timu hizo, ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Kipre Tchetche, aliyefunga mabao sita, akifuatiwa na Gwiji na Nahodha wa zamani wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’, aliyetupia mara tano.

05: Ni ushindi wa asilimia 100 ilioupata Azam FC katika mechi zote tano ilizocheza na Coastal Union kwenye Uwanja wa Azam Complex, katika mechi hizo ikifunga jumla ya mabao 15 ukiwa ni wastani wa kufunga mabao matatu kila mechi.

02: Ni idadi ya misimu ambayo Coastal Union imekaa bila kushiriki Ligi Kuu tokea iliposhuka msimu wa 2015-2016 na kurejea tena msimu huu (2018-2019).

Msimu iliposhuka ndio pekee iliyofanikiwa kuifunga Azam FC mchezo uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani, bao lao pekee likifungwa na Miraji Adam.

Matokeo msimu huu

Wakati timu hizo zikikutana, Azam FC imefanikiwa kucheza jumla ya mechi saba ikishinda mara nne na sare tatu ikiwa bado haijapoteza mchezo wowote hadi sasa ikijikusanyia jumla ya pointi 15 katika nafasi ya pili kwenye msimamo.

Coastal inayofahamika kwa jina la utani la Wagosi wa Kaya, hadi sasa ipo nafasi ya saba ikiwa na pointi 13 ikifanikiwa kucheza jumla ya mechi nane ikishinda mara tatu, sare nne na kupoteza moja iliyocheza dhidi ya Yanga.