BAADA ya kuichapa Tanzania Prisons usiku wa kuamkia leo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amewapa ujanja nyota wake wa kutilia mkazo mechi zote zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) kuhakikisha wanashinda.

Azam FC imerejea nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 15 baada ya kuichapa Prisons bao 1-0 lililofungwa na Yahya Zayd, ukiwa ni ushindi wake wa nne kwenye msimu huu wa ligi katika mechi saba ilizocheza hadi sasa, mechi nyingine tatu ikitoka sare.

Baada ya mchezo huo, Azam FC itashuka tena kwenye Uwanja wa Azam Complex Jumatatu ijayo kuvaana na Coastal Union, kabla ya ligi kusimama kupisha mechi za kufuzu Mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon, Tanzania ‘Taifa Stars’ ikikipiga na Capeverde Oktoba 12 ugenini na Oktoba 16 nyumbani.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Pluijm alisema wanaenda kucheza na Coastal Union wakitambua kuwa sio timu mbaya akidai ni timu inayocheza kwa kasi sana mipira mirefu.

“Ni mechi nyingine ya nguvu hii ni timu (Coastal Union) inayocheza kwa kasi sana mipira mirefu, kama una wachezaji warefu inakupa ugumu sana, unatakiwa kushinda kuwania mipira na kushinda pia mipira wanayoiokoa (second ball).

“Coastal Union sio timu mbaya wamekuwa wakipata matokeo mazuri, kwangu mimi jambo la muhimu ni tunatakiwa kuendelea kuwa na malengo na kucheza mechi zote kwa kuzitilia mkazo na kwenda wote kuhakikisha tunachukua tena pointi tatu,” alisema.

Akizungumzia mchezo uliopita dhidi ya Prisons, Pluijm alisema kuwa vijana wake wote walifanya kazi nzuri kwa kucheza vema na kutengeneza nafasi nyingi huku akimsifia mshambuliaji wake kinda, Yahya Zayd, kwa kazi nzuri aliyofanya.

“Nafikiri tulicheza kwa kiwango kizuri zaidi kwenye kipindi cha kwanza na tukarudia pia kipindi cha pili, nikielezea hasa kipindi cha kwanza mwamuzi alishindwa kutupa penalti ya wazi ukiacha hilo tulitengeneza nafasi kadhaa na kipindi cha pili tulifanya hivyo pia na tukafunga bao moja.

“Tungeweza kuua mchezo kwa mkwaju wa penalti (uliokoswa na Agrey Moris) ungefanya matokeo kuwa 2-0 lakini jambo la muhimu sana ni kuwa tumetengeza nafasi na sasa kilichobakia kwao ni kufunga kwa kuzitumia nafasi zetu,” alisema.

Akimzungumzia Zayd, aliongeza kuwa; “Angalia ni mchezaji mwenye akili sana na mchezaji mwenye kipaji lakini ukiweka kando kipaji hicho hasa kwenye ligi ya Tanzania unatakiwa kupambana, kupambana unatakiwa kupambania mpira, kushinda mpira unaookolewa na wapinzani (second ball) na hivyo ndio vitu ninavyojaribu kuviongeza kwake, lakini nimefurahishwa na kiwango chake.”

Katika hatua nyingine, pia alielezea kufurahishwa na hali ya kupambana na mshambuliaji Donald Ngoma, aliyekuwa akicheza mechi yake ya pili jana akidai hatua kwa hatua atakuwa vizuri.

“Najua kama Ngoma anacheza najua kuwa wanatambua uwepo wake (wapinzani) na hili ni jambo muhimu na najua ametimiza wajibu wake hivi sasa ndio ameanza kucheza nadhani amefanya kile anachopaswa na hatua kwa hatua atafikia kwenye kiwango chake lakini amecheza kwa roho nzuri ya kupambana,” alisema.

Kuelekea mchezo ujao wa Coastal Union, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza rasmi mazoezi kesho mara baada ya mapumziko ya leo, isipokuwa wachezaji sita walioitwa Taifa Stars, ambao wataungana kwenye mazoezi ya pamoja na wachezaji waliobaki siku moja kabla ya mchezo huo.