KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya kweli usiku huu baada ya kuichapa Tanzania Prisons bao 1-0, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 15 ikizidiwa pointi moja na Mtibwa Sugar yenye 16, ambayo imecheza mchezo mmoja zaidi.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake, timu zote zikicheza kwa kasi lakini Azam FC ikionekana kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo, ambapo kwa mara ya kwanza kwenye safu ya ushambuliaji, Donald Ngoma na Yahya Zayd, walianza pamoja katika kikosi cha kwanza.

Nyota wa mchezo huo kwa upande wa Azam FC walikuwa ni mshambuliaji Zayd, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambao walifanikiwa kumiliki eneo la kushambulia la timu hiyo wakishirikiana na Ngoma na Mahundi.

Azam FC ililazimika kusubiria hadi dakika ya 58 kuweza kuandika bao la ushindi lililofungwa na Zayd, aliyepiga shuti lililobabatiza mabeki wa Prisons na kujaa wavuni akiunasa mpira uliowagonga mabeki kufuatia shuti la beki wa kushoto wa Azam FC, Nickolas Wadada.

Hilo linakuwa bao la kwanza kwa Zayd msimu huu, hadi sasa Azam FC ikiwa imeshacheza mechi saba za ligi ikishinda mara nne na kutoka sare mara tatu ikiwa haijapoteza mchezo wowote.

Mabingwa hao wangeweza kuongeza bao jingine dakika ya 72 baada ya kupata penalti, ambayo ilikoswa na Nahodha Agrey Moris kufuatia kupanguliwa na kipa wa Prisons, Aron Kalambo. Penalti hiyo ilitokana na Ngoma kuangushwa kwenye eneo la hatari.

Mabadiliko ya dakika 25 za mwisho ya kuingia Ramadhan Singano na Mbaraka Yusuph, yalizidi kuiongezea nguvu Azam FC kwenye eneo la ushambuliaji lakini tatizo la kukosa umakini liliinyima mabao zaidi ya kuandikisha ushindi mnono.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kurejea mazoezini Alhamisi ijayo jioni kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Coastal Union utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumatatu ijayo saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Hassan Mwasapili, Abdallah Kheri, Agrey Moris (C), Frank Domayo, Joseph Mahundi, Salum Abubakar, Donald Ngoma/Mbaraka dk 77, Yahya Zayd, Enock Atta/Singano dk 65