KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa na kibarua kizito kuvaana na Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaama kesho Jumanne saa 1.00 usiku.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi ya kutoka suluhu dhidi ya Lipuli katika mechi yake iliyopita, mechi ambayo ilishuhudiwa urejeo wa mshambuliaji Donald Ngoma, aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu aliyesajiliwa msimu huu akitokea Yanga kwa usajili huru.

Benchi la ufundi la timu hiyo linatarajia kuendelea kumpa dakika nyingi za kucheza Mzimbabwe huyo ambaye alicheza dakika 28 za mwisho za mchezo uliopita akionekana kufanya vema tofauti na matarajio ya wengi baada ya kuwa nje takribani mwaka mmoja.

Mabingwa hao wa ligi msimu 2013/2014 wanaodhaminiwa na African Fruti, Uhai Drinking Water na Tradegents Tanzania Limited, wamekuwa kwenye maandalizi makali kuhakikisha wanavuna pointi zote katika mchezo huo ili kuendelea kujiweka sawa kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi, akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo uliopita alisema watahakikisha wanashinda mchezo huo.

“Wachezaji wanalijua hilo tuna jukumu letu kushinda hatuwezi kusogea kwenye msimamo wa ligi bila kupata pointi tatu kwa hiyo nadhani hii imeisha (Lipuli) tunaisahau na tunangoja inayokuja (Tanzania Prisons),” alisema

Wachezaji pekee watakaokosekana kwenye mchezo huo kwa upande wa Azam FC, ni beki Yakubu Mohammed, ambaye kwa sasa anatafuta ufiti wa kurejea kwenye mechi ya ushindani akitokea kwenye majeruhi pamoja na winga Joseph Kimwaga, anayesumbuliwa na maumivu ya goti.

Nyota mwingine atakayeendelea kukosekana ni beki wa kushoto, Bruce Kangwa, ambaye ana ruhusu maalumu ya kwenda kuhudhuria mazishi ya kaka yake aliyefariki dunia wiki moja iliyopita kwa ajali ya kugongwa na gari nchini Afrika Kusini.

Rekodi za timu hizo

Mpaka sasa kihistoria timu hizo zimekutana mara 16 kwenye mechi za ligi, Azam FC ikiwa na rekodi ya kushinda mara saba, Prisons yenyewe mara tatu ikiibuka kidedea huku ikishuhudiwa mechi sita zikiisha kwa sare.

Azam FC ilinawiri vilivyo kwenye mchezo wa mwisho baina ya timu hizo uliofanyika uwanjani hapo baada ya kuibuka na ushindi mabao 4-1, ikishuhudiwa mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Shaaban Idd, aliyetimkia CD Tenerife ya Hispania, akitupia hat-trick na bao jingine likifungwa na Nahodha Msaidizi, Frank Domayo.

Mchezo wa awali ugenini kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Azam FC ilishinda mabao 2-0 yaliyofungwa na mshambuliaji Yahya Zayd na chipukizi Paul Peter, ambaye kwa sasa ni majeruhi.

Ushindi huo ulimaanisha kuwa kwa msimu wa pili mfululizo, Azam FC ilijiandikia rekodi ya kuvuna pointi zote sita katika mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya Maafande hao wa Magereza.

Jumla ya mabao 29 yamefungwa na timu hizo katika mechi zote 16 walizokutana, Azam FC imefunga 18 ikiwa ni wastani wa 1.75 wa kufunga mabao katika kila mchezo huku Prisons ikitikisa nyavu za matajiri hao mara 11.

Ushindi utamaanisha

Ushindi wowote kwa Azam FC iliyocheza mechi saba mpaka sasa za ligi, utazidi kuisogeza kwenye nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa ligi kwani itafikisha jumla ya pointi 15 huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi.