BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Yakubu Mohammed, juzi alipewa programu maalumu ya kucheza mechi ya kujiweka fiti wakati timu ya vijana ya timu hiyo (Azam U-20) ikikipiga na Mbande FC.

Yakubu aliyerejea mazoezini na wenzake Jumanne iliyopita akitokea kwenye majeraha ya muda mrefu ya kifundo cha mguu wa kulia, alicheza dakika 45 za kipindi cha kwanza akionekana kuanza vizuri akiiongoza Azam U-20 kuichapa Mbande mabao 3-1.

Ukiondoa Yakubu, wachezaji wengine wa timu kubwa ya Azam FC waliocheza mchezo huo ni washambuliaji Mbaraka Yusuph na Wazir Junior, ambao wote walifunga mabao safi.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, alikuwa jukwaani kumshuhudia Yakubu saambamba na wachezaji wengine hao wa timu kubwa, ikiwa ni katika kuwaangalia kiufundi na ufiti kwa ajili ya kuwatumia kwenye mechi zake zijazo za timu hiyo.

Beki huyo raia wa Ghana, amekaa nje ya dimba takribani miezi saba akiuguza majeraha hayo aliyopata wakati Azam FC ikiichapa KMC mabao 3-1 kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Ujio wake unazidi kuimarisha zaidi sehemu ya ulinzi ya Azam FC, ambayo ina mabeki wengine wa kati bora kabisa waliopo timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Nahodha Agrey Moris, Abdallah Kheri, David Mwantika na chipukizi Oscar Masai, aliyepandishwa kutoka timu ya vijana (Azam U-20).