KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC,  imelazimishwa sare ya bila kufungana na Lipuli katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex leo usiku.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 12 sawa na Yanga zote zikiwa nafasi tatu za juu kileleni ikiwa Mbao yenye pointi 14.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake, Azam FC ikianza kwa kasi kipindi cha kwanza na kukosa nafasi mbili za wazi dakika tano za mwnao kupitia kwaTafadzwa Kutinyu na Danny Lyanga.

Dakika ya 15 Lyanga aliunasa mpira uliookolewa vibaya na mabeki wa Lipuli na kupiga shuti zuri lililotoka pembeni kidogo ya lango.

Nafasi nyingine muhimu ya Azam FC ilikuwa ni kuelekea dakika 20 za mwisho za kipindi cha kwanza, ambapo mpira mzuri wa adhabu ndogo uliopigwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ ulipanguliwa na kipa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwenzake, kipindi cha pili Azam FC iliendelea na kasi yake lakini ugumu ulikuwa ni namna ya kuipenya safu ngumu ya ulinzi ya Lipuli.

Dakika ya 62,  ilishuhudiwa kwa mara ya kwanza baada ya mwaka mmoja kupita,  mshambuliaji Donald Ngoma, akiingia kucheza mechi akitoka kwenye majeraha huku pia akiichezea Azam FC mechi yake ya kwanza tokea asajiliwe msimu huu akitokea Yanga.

Ngoma aliingia kuchukua nafasi ya Mudathir Yahya, ambaye alionekana kuelewana vema na mshambuliaji mwingine aliyeingia baadaye Yahya Zayd wakionekana kuisumbua vema safu ya ulinzi ya Lipuli.

Kama waamuzi wangekuwa makini wangeweza kuipa penalti Azam FC dakika 15 za mwisho za mchezo huo baada ya kipa wa Lipuli kumparasa kwa mikono Ngoma baada ya kuutanguliza mpira mbele mpira wakati akiwa kwenye harakati za kufunga.

Kama si umaridadi wa kipa wa Lipuli huenda Kutinyu angeipatia bao la uongozi Azam FC kuelekea dakika 10 za mwisho za mchezo huo, baada ya kupiga kichwa kizuri kilichopanguliwa na kipa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Hiyo ni sare ya kwanza kwa Azam FC msimu huu kwenye uwanja wake wa nyumbani, ikiwa ni ya tatu katika mechi sita ilizocheza hadi sasa kati ya hizo ikiwa imeshinda mara tatu pia.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho kabla ya kurejea mazoezini keshokutwa Jumapili kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Tanzania Prisons utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumanne ijayo saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Hassan Mwasapili, Abdallah Kheri, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya/Donald Ngoma dk 62, Joseph Mahundi, Frank Domayo, Danny Lyanga/Yahya Zayd dk 65, Tafadzwa Kutinyu, Ramadhan Singano/Salum Abubakar dk 75