BAADA ya kucheza mechi tatu mfululizo ugenini, kesho Ijumaa Azam FC itarejea nyumbani kukipiga na Lipuli katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) unaotarajia kufanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

Azam FC inarejea nyumbani ikitoka kuichapa Alliance bao 1-0, lililofungwa na Tafadzwa Kutinyu, baada ya awali kutoka sare mbili dhidi ya Mwadui (1-1), Biashara United (0-0) zote zikiwa ni mechi tatu za ugenini.

Kikosi hicho kimekuwa kwenye maandalizi makali tokea Jumanne kiliporejea jijini Dar es Salaam, wachezaji wakionekana na morali ya juu mazoezini tayari kwa kuendelea kuvuna pointi tatu muhimu katika uwanja wake wa nyumbani.

Huo utakuwa ni mchezo wa tatu wa ligi nyumbani msimu huu kwa Azam FC, miwili ya awali ikizichapa Mbeya City (2-0) na Ndanda (3-0) kabla ya kuhamia ugenini ikishinda mmoja na sare mbili.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na habari njema za kurejea mazoezini kwa beki wake, Yakubu Mohammed, ambaye muda si mrefu anatarajia kuanza kuonekana kwenye mechi za ushindani sambamba na mshambuliaji Donald Ngoma, ambao kwa pamoja wanaendelea kujiweka fiti.

Kauli ya Kocha

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amesema kuwa watafanya kila kitu kuhakikisha wanavuna pointi tatu kwenye uwanja wa nyumbani.

“Unapocheza nyumbani basi unapaswa kuchukua pointi zako tatu na tutafanya kila kitu kiwezekanavyo kupata pointi tatu, naijua Lipuli sio timu mbaya kabisa lakini tunatakiwa kuwaonyesha mashabiki wetu kwamba sisi ni kweli tunataka kwenda nafasi ya juu kwenye ligi,” alisema.

Alisema wachezaji wake wanamorali ya hali ya juu baada ya kutoka kupata ushindi kwenye mchezo uliopita huku akidai hawatamdharaua mpinzani wao yoyote atakayekuja mbele yao.

“Kila mmoja anatakiwa kuweka mkazo dakika 90 na kucheza kwa umakini na uamuzi ndani ya dakika 90 hilo ndilo natarajia kwa wachezaji wangu,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Tunajaribu kuwa timu nzuri, tuko pamoja kwa takribani miezi miwili tu nadhani hatua kwa hatua mambo yatakwenda vema, wachezaji wametoka kwenye majeruhi (Yakubu na Ngoma) hivi sasa wamejiunga kwenye mazoezi hilo ni jambo la muhimu pia, na kutakuwa na ushindani wa namba kwa ajili ya nafasi.”

Azam FC v Lipuli H2H

Hiyo itakuwa ni mechi ya tatu kwa timu hizo kukutana kwenye ligi, mechi mbili za awali msimu uliopita Azam FC ikishinda mmoja na kutoka suluhu ugenini kwenye Uwanja wa Samora, mkoani Iringa

Mechi iliyoshinda iliichapa Lipuli bao 1-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, lililowekwa kimiani na mshambuliaji Mbaraka Yusuph, aliyemalizia kazi nzuri iliyofanywa na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Himid Mao ‘Ninja’, aliyehamia Petrojet ya Misri.