JUMLA ya wachezaji nane wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, wameitwa kujiunga na timu mbalimbali za Taifa kwa ajili ya mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.

Wachezaji sita kati ya hao wameitwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayojiandaa na mechi mbili dhidi ya Visiwa vya Capeverde, zitakazofanyika Oktoba 12 ugenini na Oktoba 16 jijini Dar es Salaam.

Nyota hao ni mabeki Agrey Moris, David Mwantika, Abdallah Kheri, viungo Mudathir Yahya, Frank Domayo ‘Chumvi’ na mshambuliaji Yahya Zayd, wanaounda kikosi cha wachezaji 30 walioitwa na Kocha Mkuu, Emmanuel Amunike.

Kwa upande wa wachezaji wa nje ya nchi walioitwa na timu zao wakitokea Azam FC, ni beki wa kulia Nickolas Wadada, aliyejumuishwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ itakayokuwa ikijiandaa kukipiga na Lesotho.

Kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu, naye ameitwa timu ya Taifa ya Zimbabwe ‘The Warriors’, inayotarajia kucheza mechi mbili dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo).

Kikosi kamili cha Taifa Stars, ambacho kina nafasi nzuri ya kufuzu fainali hizo kinaundwa na makipa Aishi Manula (Simba SC), Beno Kakolanya (Yanga SC) na Mohamed Abdulahman (JKT Tanzania).

Mabeki ni Hassan Kessy (Nkana FC/Zambia), Shomari Kapombe (Simba SC), Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Gardiel Michael (Yanga SC), Paulo Ngalema (Lipuli FC), Ally Sonso (Lipuli FC), Agrey Moris (Azam FC), David Mwantika (Azam FC), Abdallah Kheri (Azam FC), Kelvin Yondani (Yanga SC), Andrew Vincent (Yanga SC) na Abdi Banda (Baroka FC).

Viungo ni Nahodha Msaidizi, Himid Mao (Petrojet/Misri), Simon Msuva (Difaa Hassan El –Jadida/Morocco), Mudathir Yahya (Yanga SC), Frank Domayo (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Feisal Salum (Yanga SC), Salum Kihimbwa (Mtibwa Sugar) na Farid Mussa (CD Tenerife/Hispania).

Washambuliaji ni Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Thomas Ulimwemgu (Al Hilal/Sudan), John Bocco (Simba SC), Yahya Zayd (Azam), Kelvin Sabato (Mtibwa Sugar), Rashid Mandawa (BDF XI/Botswana) na Shaaban Iddi Chilunda (CD Tenerife/Hispania).