KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Tafadzwa Kutinyu, amejiwekea malengo ya kuendelea kufunga katika mechi zijazo za timu hiyo ili kuhakikisha anaipa ushindi timu hiyo akishirikiana na wachezaji wenzake kikosini.

Kutinyu hadi sasa ndiye kinara wa mabao wa Azam FC katika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) akiwa na mabao matatu katika mechi nne kati ya tano alizoichezea timu hiyo hadi sasa.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co,tz, Kutinyu alisema anajisikia furaha kuendelea kufunga akidai kitu hicho ni kizuri kwenye timu kwa kuwa wanaendelea kukusanya pointi tatu.

“Tunapambana, kila mmoja anapambana kwa ajili ya timu hivyo sio kuhusu mimi kwa kuwa nafunga hii ni kwa ajili ya kila mmoja anayefanya kazi kwa bidii, hivyo shukrani kwa kila mmoja kwa mchango kwa ajili ya timu,” alisema.

Akizungumzia rekodi yake hiyo ya mabao, Mzimbabwe huyo alisema kuwa; “Hadi sasa mimi najisikia furaha sana na nahitaji zaidi, ninaomba kwa Mungu na Mungu atatubariki na mimi kuendelea kufunga na timu itapata pointi zote na mwisho wa siku tutaisaidia timu kupata mafanikio.”

Alisema hakuna siri yoyote ya yeye kuendelea kufanya vizuri na kufunga mabao akidai siri kubwa iliyopo ni wao kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya timu.

“Sio kuhusu mtu mmoja, tunasaidiana kila mmoja kama mtu mmoja akiwa yupo chini tunamsaidia na kumpandisha juu, kwa hiyo tunasaidiana kila mmoja kwa ajili ya kupata pointi zote kwa kila mechi, kwa hiyo tunamshukuru kila mmoja kwenye timu aliye nje au ndani, kwa sababu tunasaidiana kila siku,” alisema.

Nyota huyo aliyemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Zimbabwe ‘The Warriors’, amefunga mabao hayo matatu wakati Azam FC ikiichapa Ndanda 3-0, mechi aliyofunga mawili pamoja na ule wa ugenini dhidi ya Alliance, akitupia bao pekee la ushindi.