BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Yakubu Mohammed, aliyekuwa majeruhi amerejea rasmi mazoezini na wenzake akiwa na kasi mpya tayari kuipigania timu hiyo kuelekea mechi zijazo.

Yakubu amekaa nje ya dimba takribani miezi saba akiuguza majeraha ya kifundo cha mguu wa kulia aliyopata wakati Azam FC ikiichapa KMC mabao 3-1 kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Beki huyo anarejea kuimarisha zaidi sehemu ya ulinzi ya Azam FC, ambayo ina mabeki wengine wa kati wazuri akiwemo Nahodha Agrey Moris, Abdallah Kheri, David Mwantika na chipukizi Oscar Masai, aliyepandishwa kutoka timu ya vijana (Azam U-20).

Akizungumzia urejeo wake mara baada ya kumalizika kwa mazoezi yake ya kwanza na wenzake leo Jumanne usiku, alimshukuru Mwenyezi Mungu na uongozi wa Azam FC kwa kusaidia kurejea kwake tena dimbani.

“Kwa kweli ninachoweza kusema, nasema Alhamdulillah Alhamdulillah Alhamdulillah najisikia vizuri zaidi, kabla ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunirudisha baada ya miezi saba najisikia vizuri zaidi sasa.

“Napeleka shukrani pia kwa uongozi kwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwangu kwa ajili ya kwenda kwa mtaalamu wa viungo ‘physio’ kabla ya kwenda Afrika Kusini na kurudi nilikuwa nafanya programu ya matibabu ‘physiotherapy’ na ilikuwa ni nzito sana, ninachoweza kusema ni Alhamdulillah Alhamdulillah najisikia furaha sana hivi sasa nafanya mazoezi na timu,” alisema.

Alivyojipanga

Beki huyo aliyesajiliwa misimu miwili iliyopita akitokea Aduana Stars ya Ghana, alisema anachoangalia hivi sasa ni kufanya kazi kwa bidii ili kujumuishwa kwenye kikosi cha kwanza na Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm.

“Ila kwa sasa kwa mechi inayokuja Ijumaa (vs Lipuli) sifikiri kama naweza kuwa kwenye orodha kwa sababu haya ni mazoezi yangu ya kwanza na timu, hivyo Inshallah tutaona baada ya mechi ya Ijumaa.

“Baada ya mechi ijayo tutaona kitu gani kocha atafanya, kama ataniweka kikosini Alhamdulillah na kama sitakuwepo basi nitaendelea kufanya kazi kwa bidii kwa sababu nimerejea baada ya miezi saba,” alisema.

Awapa tano mashabiki

Aidha Yakubu alichukua fursa kuwashukuru mashabiki wa Azam FC kwa sapoti kubwa waliyokuwa wakimpa wakati akiwa mgonjwa na kuwaahidi wataanza kumuona dimbani hivi karibuni.

“Kwa kweli najua mashabiki watakuwa na furaha kuniona nafanya mazoezi kwa sababu nilipokuwa nje walikuwa na huzuni sana walitaka nirejee na kitu ninachowambia mashabiki nawashukuru sana kwa sala zao na namna walivyokuwa wananitia moyo.

“Kila mara walivyokuwa wanakuja kuangalia mechi zetu hapa walikuwa wananihamasisha Yakubu tunakuhitaji tunakuhitaji na leo nawaambia wote nawashukuru sana, nathamini upendo wao, maombi yao na kila kitu, Alhamdulillah nafanya mazoezi sasa hivi, hivyo wataniona muda si mrefu, nitaanza kucheza hivi karibuni Inshallah,” alimaliza Mohammed.

Ukiachana na Yakubu, mshambuliaji mwingine wa Azam FC, Donald Ngoma, naye anaendelea vema na programu ya kujiweka sawa akifanya mazoezi na wachezaji wenzake, ambapo muda wowote kuanzia sasa anatarajia kuanza kuonekana kwenye mechi za ushindani.