KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Hans Van Der Pluijm, ametoa angalizo kwa wachezaji wake akisema kuwa inahitajika utayari kuelekea mchezo ujao dhidi Lipuli.

Mara baada ya Azam FC kumaliza mechi zake tatu za Kanda ya Ziwa, sasa itarejea nyumbani Ijumaa hii kuvaana na Lupuli katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi saa 1.00 usiku.

Azam FC ilihitimisha mechi za kanda hiyo, kwa kuichapa Alliance bao 1-0 lililofungwa na Tafadzwa Kutinyu, awali ilicheza michezo mingine miwili na kutoka sare dhidi ya Mwadui (1-1) na Biashara United (0-0).

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Pluijm amekiri ugumu wa wapinzani wao kuelekea mchezo huo huku akidai wanatakiwa kujiandaa vema ili kuweza kuvuna ushindi mwingine Alhamisi.

“Unajua kuwa kila timu dhidi ya Azam, wanacheza asilimia 50 zaidi ya mechi nyingine tunatakiwa kuwa tayari kwa ajili ya hilo na kujiandaa vema,” alisema.

Ripoti Kanda ya Ziwa

Akitoa ripoti yake ya mechi tatu zilizopita walizocheza Kanda ya Ziwa, Mholanzi huyo alisema wangeweza kuvuna pointi tisa kama waamuzi wangekuwa makini.

“Niwe muwazi na nimeshaliongea hili kabla pia na waandishi wengine, nafikiri kama waamuzi wangetenda haki katika mechi tatu tulizocheza tungepata pointi tisa lakini yote hutokea kwenye mechi, tunatakiwa kusahau yote na kuyaacha nyuma kwa sababu ni ngumu kuyarudisha,” alisema.

Kuelekea mchezo na Lipuli, kikosi cha Azam FC kilichorejea usiku wa kuamkia leo Jumanne kikitokea mkoani Mwanza, kinatarajia kuanza rasmi mazoezi leo saa 2 usiku kujiandaa na mtanange huo.