BAO pekee lililofungwa na kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Tafadzwa Kutinyu, limetosha kuipa pointi tatu muhimu timu hiyo dhidi ya Alliance jioni ya leo.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) ulifanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ukiwa ni wa raundi ya sita ukichezeshwa na mwamuzi Jonesia Rukyaa kutoka mkoani Kagera.

Timu zote ziliweza kuonyeshana umwamba, Azam FC ikionekana kucheza vema zaidi kipindi cha pili hasa baada ya kuingia kwa mshambuliaji Mbaraka Yusuph, aliyeonekana kuisumbua safu ya ulinzi ya Alliance.

Azam FC ilibidi isubiri hadi dakika ya 59 kuweza kuandika bao hilo la ushindi, lililofungwa na Kutinyu kwa kichwa akitumia pande safi alilopenyezewa na Mbaraka.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 11 kwenye msimamo wa ligi, ikifanikiwa kuondoka na pointi tano kati ya tisa katika mechi za Kanda ya Ziwa, baada ya kutoka sare mbili dhidi ya Mwadui (1-1), Biashara United (0-0) kabla ya kuichapa Alliance.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka jijini Mwanza kesho alfajiri tayari kurejea jijini Dar es Salaam kujiandaa na mtanange ujao dhidi ya Lipuli utakofanyika Uwanja wa Azam Complex Septemba 27 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Hassan Mwasapili, Abdallah Kheri, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Salum Abubakar dk 72, Frank Domayo, Danny Lyanga/Mbaraka Yusuph dk 46, Tafadzwa Kutinyu, Ramadhan Singano/Enock Atta dk 46