KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa kibaruani kesho Jumapili kuvaana na Alliance ya huko katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, mjini Mwanza.

Huo utakuwa ni mchezo wa kwanza kwa timu hizo kukutana kihistoria, ambapo Alliance ni miongoni mwa timu sita zilizopanda daraja msimu huu.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kujikusanyia pointi nane ikizidiwa pointi mbili na Mbao iliyokileleni lakini ikicheza mchezo mmoja zaidi ya matajiri hao.

Wababe hao kutoka viunga vya Azam Complex, watakuwa wakisaka ushindi wa kwanza ugenini msimu huu baada ya mechi mbili zilizopita kutoka sare dhidi ya Mwadui (1-1) na Biashara United (0-0).

Hadi sasa Alliance ikiwa imecheza mechi tano za ligi, bado haijafanikiwa kuvuna ushindi wowote, ikiwa imeambulia sare moja ilipocheza na African Lyon (1-1) na kupoteza mechi nne.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi, akizungumza baada ya mchezo uliopita, alisema wanaenda kucheza Alliance wakiwa na lengo la kuzoa pointi zote tatu ili kujiweka sawa kwenye msimamo wa ligi.

Miongoni mwa wachezaji wote wa Azam FC waliosafiri na timu kwenye mechi za Kanda ya Ziwa, katika mchezo huo timu hiyo itamkosa beki wa kushoto, Bruce Kangwa, aliyesafiri juzi kwa ajili ya mazishi ya kaka yake aliyefariki nchini Afrika Kusini baada ya kugongwa na gari.

Ni wazi sasa nafasi yake itazibwa na beki mwenzake kikosini Hassan Mwasapili, aliyesajiliwa msimu huu akitokea Mbeya City, aliyoichezea kwa muda mrefu tokea wakiwa Daraja la Kwanza na kupanda Ligi Kuu mwaka 2013.

Huo utakuwa ni mchezo wa tano kwa Azam FC kucheza msimu huu, mechi nne za awali imeshinda mbili kwa kuzichapa Mbeya City (2-0) na Ndanda (3-0) huku ikitoka sare mara mbili dhidi ya Mwadui na Biashara United.