KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanikiwa kuvuna pointi nyingine moja ugenini baada ya kutoka suluhu dhidi ya Biashara katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Karume, mjini Musoma, Mara jioni ya leo.

Hiyo ni sare ya pili ya ugenini mfululizo kwa Azam FC baada ya Ijumaa iliyopita kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mwadui, na sasa ikifikisha jumla ya pointi nane.

Azam FC ilianza vema mchezo huo na dakika ya nne tu, winga Ramadhan Singano ‘Messi’, alipiga krosi nzuri lakini mpira wa kichwa uliopigwa na mshambuliaji Danny Lyanga, ulikatika na kuokolewa na mabeki wa Biashara.

Kuelekea mwishoni mwa kipindi cha kwanza, Azam FC ilipoteza nafasi nyingine tatu za kufunga mabao kupitia kwa Lyanga, Tafadzwa Kutinyu na Joseph Mahundi na kufanya timu zote mbili ziende mapumziko zikiwa hazijafungana.

Mabadiliko ya kuingia washambuliaji Yahya Zayd na Mbaraka Yusuph, kwa nyakati tofauti mwanzoni mwa kipindi cha pili, yaliongeza uhai kwenye safu ya ushambuliaji ya Azam FC ambayo ilifanya mashambulizi takribani matatu makali langoni mwa Biashara.

Mwamuzi wa mchezo huo, Shomari Lawi, aliinyima bao la wazi Azam FC dakika ya 80, baada ya mshambuliaji Yahya Zayd, kupiga shuti zuri lililogonga mwamba wa juu na kudundia ndani kabla ya mpira kurejea tena uwanjani.

Hilo ni bao la tatu mfululizo ambalo Azam FC inanyimwa na waamuzi katika mechi mbili mfululizo, itakumbukwa katika mchezo uliopita dhidi ya Mwadui mabao yaliyofungwa na Lyanga na Singano yalikataliwa na Azam FC kutoka sare ya bao 1-1.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka mjini Musoma kesho asubuhi kuelekea mkoani Mwanza kwa ajili ya kuvaana na Alliance ya huko, mchezo utakaofanyika Jumapili hii kwenye Uwanja wa Nyamagana.

Kikosi cha Azam FC leo:

Mwadini Ally, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, David Mwantika, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Joseph Mahundi, Salum Abubakar, Danny Lyanga/Mbaraka Yusuph dk 68, Tafadzwa Kutinyu/Yahya Zayd dk 58, Ramadhan Singano/Idd Kipagwile dk 80