WIKI hii Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa na mtihani mtihani mzito wa kuhahakikisha inaondoka na pointi sita katika mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) zilizobakia Kanda ya Ziwa.

Baada ya kucheza na Mwadui na kutoka sare ya bao 1-1, sasa imewasili mkoani Mara siku mbili zilizopita, kuhakikisha inavuna pointi tatu muhimu keshokutwa Jumatano dhidi ya Biashara United kabla ya kuelekea mkoani Mwanza kuvuna tatu nyingine itakapokipiga na Alliance Jumapili hii.

Wachezaji wote wa Azam FC wako katika hali nzuri, ambapo tayari kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu, ameshajiunga na timu akitokea kwenye majukumu ya timu ya Taifa ya Zimbabwe ‘The Warriors’.

Kikosi hicho chini ya Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm, jana kilianza mazoezi ya kwanza mjini Musoma kwenye Uwanja wa Karume utakaochezewa mchezo huo, ambao unasubiriwa na mashabiki wengi wa soka mkoani humo.

Tayari Pluijm ameshaweka wazi kuwa, wanaingia kwenye mechi hizo mbili kuhakikisha wanavuna alama tatu katika kila mchezo japo akikiri kuwa mpira una matokeo matatu, kushinda, kutoka sare na kufungwa.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza Azam FC kutua mkoani Mara, Musoma, kucheza soka baada ya kupanda daraja kwa timu hiyo ya huko msimu uliopita wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

  Hadi sasa kwenye msimamo wa ligi, Azam FC imefanikiwa kujikusanyia jumla ya pointi saba katika nafasi ya pili kwenye msimamo ikizidiwa pointi moja na JKT Tanzania iliyofikisha nane lakini ikicheza mechi moja zaidi ya matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.